Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Naibu Waziri Mgalu awapa somo wazalishaji vifaa vya umeme

Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wazalishaji wa vifaa vya umeme wametakiwa kutoiangusha Serikali kufuatia agizo lake la kuzuia vifaa vya nishati hiyo kutoingizwa nchini.

Badala yake wametakiwa kutumia fursa hiyo kuzalisha vifaa vyenye ubora wa kimataifa huku suala la usalama likizingatiwa.

Hayo yameelezwa leo Septemba 26, 2018 na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alipotembelea kiwanda cha kuzalisha vifaa vya umeme cha Africab jijini Dar es Salaam.

Mgalu amekwenda kwenye kiwanda hicho kuangalia uwezo wake katika uzalishaji.

Amesema Serikali iliona hakuna sababu ya vifaa vinavyoweza kuzalishwa nchini kuagizwa nje hivyo ni jukumu la wazalishaji wa ndani kuhakikisha wanaitendea haki fursa hiyo.

"Serikali imetoa agizo vifaa visiingie nchini sasa  lazima tupite kwenye viwanda tulivyonavyo kuona uwezo wake katika uzalishaji,” amesema.

Mgalu ambaye ni mbunge wa viti maalum (CCM) amesema, “Tuna miradi mingi sasa isijwe ikawa inashindwa kutekelezeka kwa kisingizio cha vifaa, nimejionea mwenyewe hapa vifaa vipo vya kutosha.”

Kwa upande wake, mkuu wa masoko wa kiwanda hicho, David Tarimo amesema licha ya uwezo mkubwa katika uzalishaji bado kuna changamoto ya soko.

“Vifaa tunavyo vingi na tunazingatia sana ubora katika uzalishaji tatizo bado soko si kubwa, wahitaji wanaamini katika bidhaa za nje," amesema.

Amesema kiwanda hicho kinazalisha transfoma za kuzalisha umeme, mabomba na vifaa vingine mbalimbali vya kusambazia umeme.

Chanzo: mwananchi.co.tz