Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nafasi ya TAEC kuinua sekta ya kilimo, ufugaji na maji nchini

F1cb2a1021aab47854750ee57118dc13 Nafasi ya TAEC kuinua sekta ya kilimo, ufugaji na maji nchini

Tue, 15 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission-TAEC) ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 7 ya mwaka 2003. Awali tume hiyo ilijulikana kama Tume ya Taifa ya Mionzi iliyoanzishwa kisheria mwaka 1983.

Majukumu makubwa ya tume hiyo ni kudhibiti matumizi sahihi ya mionzi nchini, kuhamasisha na kupanua matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia na kutoa ushauri na taarifa mbalimbali za sayansi na teknolojia ya nyuklia.

Uhusiano wa majukumu hayo na masuala ya mionzi na nyuklia ndio hasa sababu ya watu wengi kudhani kuwa tume hiyo inahusika na mabomu na vitu vya hatari kama hivyo huku baadhi ya watu zamani wakiihusisha na wanyonya dam una kuifanya iogopwe na wengi hasa wakazi walioishi karibu na ofisi zake mkoani Arusha.

Hata hivyo, tume hiyo haihusiki na utengenezaji wa mabomu bali kinachofanana na kazi hiyo, ni lile jukumu lao kubwa la kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini na kutoa leseni kwa kampuni na taasisi zinazojihusisha na amsuala ya mionzi ikiwamo wachimbaji wa madini yenye viashiria vya mionzi.

Mbali na majukumu hayo, tume hiyo ni rafiki wa teknolojia zinazogusa uchumi moja kwa moja. Kwa mfano kupitia tume hiyo, serikali inashiriki katika programu za kudhibiti na kuhamasisha matumizin salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.

Programu hizo ni zile zinazofadhiliwa na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) pamoja na za kanda ya Afrika kupitia jukwaa la AFRA. Kupitia programu hizo, Tanzania imeendelea kunufaika na miradi mbalimbali katika sekta ya kilimo, afya, mifugo, maji, rasilimali wat una lishe.

Makala haya itaeleza na kuainisha sehemu ya manufaa hayo katika sekta ya kilimo, mifugo na maji.

KILIMO

Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Lazaro Busagala akizungumza hivi karibuni, Dar es Salaam katika semina kwa wahariri na waandishi wa habari waandamizi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu tume hiyo, alisema kuinua kilimo na kuongeza ajira ni moja ya jukumu lao.

Taarifa za tume hiyo zinaainisha kuwa mpunga, mahindi na mtama ni mazao matatu muhimu ya nafaka nchini ambayo uzalishaji wake umekuwa ukikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwamo magonjwa na ukame.

Mkuu wa Ofisi ya TAEC Kanda ya Mashariki, Dk Wilbroad Muhogora, anasema kwa mfano kuwa magonjwa yanayoathiri zaidi uzalishaji wa mpunga nchini ni ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama Yellow Mottle Virus (RYMV) na unadhibitiwa kwa teknolojia ya nyuklia.

Anasema ili kuudhibiti ugonjwa huo na mengine, IAEA kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (ZARI) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), zinaendesha mradi unaotumia teknolojia ya nyuklia uliowezesha kupata mbegu bora aina ya SUPA BC zinazohimili maradhi ikiwamo RYMV.

“Katika eneo la upatikanaji wa mbegu bora mbalimbali ikiwamo SUPA BC, Zanzibar imetumika sana na sasa hekta moja inatoa tani saba tofauti na tani nne za awali kabla ya kutumia mbegu hiyo,” anasema Dk Muhogora.

Dk Muhogora, akitoa mada katika semina hiyo alisema mbegu hiyo na nyingine zinazotokana na teknolojia ya nyuklia ni salama zaidi kutokana na ukweli kwamba hupatikana kwa teknolojia isiyobakisha kitu cha tofauti ndani ya mbegu au mazao.

Tume hiyo kwa kushirikiana na IAEA zimeendelea kuboresha mbegu nyingine ikiwamo za mahindi na shairi katika Taasisi ya Kilimo Seliani mkoani Arusha kwa kutumia teknolojia ya nyuklia ambapo imesaidia kupata mnegu bora za mahindi na shairi zinazohimili magonjwa mbalimbali, ukame na kutoa mavuno mengi.

Profesa Busagala anasema hatua hiyo ni kichochea kikubwa na msukumo kwa wananchi wengi hasa vijana kuingia katika kilimo kutokana na kuwapatia ajira na kuwezesha pia uchumi wa viwanda.

MIFUGO

Katika kutambua kuwa serikali imejikita katika kuboresha uzalishaji wa mifugo ikiwamo kuongeza upatikanaji wa mazao ya mifugo kama maziwa na nyama bora TAEC kwa kushirikiana na IAEA, Kituo cha Uhimilishaji wa Mifugo Arusha (NAIC) na Wakala wa Maabara za Mifugo (TVLA), wanaendelea kuzalisha mbegu bora za ng’ombe.

TAEC inasema kwamba mbegu hizo bora za ng’ombe zimekuwa zikitawanywa kwa wafugaji katika ameneo mbalimbali nchini na kupandishwa kwa njia ya uhimilishaji.

Hapa teknolojia ya nyuklia hutumia kubaini ng’ombe ambao hawajashika mimba na hatimae kupandishwa tena ndani ya siku 14. Njia hii husaidia kupunguza muda wa upandishaji n awa ng’ombe kushika mimba.

Aidha maabara ya mifugo Zanzibar imeendelea kuboreshwa ambapo mtambo wa kuzalisha gesi ya Nitrojeni unaotumika kuhifadhi mbegu za madume ya ng’ombe umekarabatiwa. Itasaidia kusafirisha mbegu za za madume hayo na kuwafikia wafugaji zikiwa hai.

“Hatua kama hizi ndizo zinapaswa kuelimishwa kwa wananchi ambao mwanzo tulipoanzishwa walidhani sisi ni kituo cha wanyonya damu, wengine wanasema tunatengeneza mabomu. Ukweli ni kwamba tunahusika na mambo ya kawaida kabisa ya kisayansi yanayogusa jamii ikiwamo kilimo kama haya,” anasema Profesa Busagala.

Anasema TAEC imeibeba dhana ya uchumi wa viwanda na kupitia matumizi ya teknolojia ya nyuklia, wanaihamasisha jamii kufahamu zaidi kazi zake na kuitumia katika kufanikisha masuala ya maendeleo ya kiuchumi hasa kilimo na mifugo.

Dk Muhogora anasema kuwa, teknolojia ya nyuklia hutumiwa pia katika gesi, mafuta, uchunguzi na utafiti wa magonjwa katika eneo la afya na maji hivyo ni sekta muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa na watu wake.

MAJI

Dk Muhogora anasema nchini kuna vituo 655 vya vyanzo salama vya maji vinavyotumia teknolojia ya nyuklia kuhakikisha yanapimwa na ni salama bila vimelea vya mionzi hatarishi ili kulinda afya ya wananchi.

Anasema serikali kupitia tume hiyo inahakikisha umma unapata taarifa sahihi kuhusu teknolojia ya nyuklia na kwa kuzingatia kuwa ni sekta mtambuka yenye kuhusisha wizara na taasisi nyingi, inaongeza nguvu ya kueleweka zaidi kwa jamii.

Awali, akifungua semina hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema TAEC imekuwa ikifanya mambo makubwa katika kulinda afya za Watanzania ikiwamo kudhibiti mionzi kwenye maji, vyakula na mazao lakini wananchi hawaijui.

“Mjenge uelewa kwa wahairiri na waandishi haw awa habari katika lugha laini inayoeleweka, mueleze wananchi nini mnafanya ili kuondoa dhana kwamba nyine mnahusika na kutengeneza mabomu,” alisema Profesa Ndalichako na kufanya hadhira iliyokuwa ikimsikiliza kucheka na wengine kutikisa vichwa wakikubaliana na anachosema.

Profesa Busagala kupitia semina hiyo, alidhihirisha wazi kuwa, TAEC inafanya mambo mengi na kusisitiza kuwa dhamira yao kubwa ni kuhusika kikamilifu katika kukuza uchumi wan chi hasa kupitia viwanda ili kushiriki kukabiliana na upungufu wa ajira nchini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz