Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NSSF yafadhili mfumo wa taarifa za Diaspora

WhatsApp Image 2022 08 26 At 4.48.18 PM 1080x640.jpeg NSSF yafadhili mfumo wa taarifa za Diaspora

Fri, 26 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wameingia makubaliano kufadhili matengenezo ya mfumo wa kidigitali wa utunzaji wa taarifa za Watanzania Wanaoishi Nje ya Nchi (DIASPORA), kwa gharama ya Shilingi milioni 50.

Makubaliano hayo, yalitiwa saini katika ofisi ndogo za wizara hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo Mkurugenzi wa Uthaminishaji, Takwimu na Usimamizi wa Hadhari, Ibrahim Maftah alimuakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba na Balozi James Bwana, Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Joseph Sokoine.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Balozi Bwana aliishukuru Bodi ya NSSF na Menejimenti kwa kukubali kufadhili matengenezo ya mfumo huo, ambao utakapokamilika utawatambua, kuwasajili na kutunza taarifa za Diaspora wa Tanzania waliotapakaa duniani kote kupata huduma muhimu kutoka kwenye Nchi yao.

Amesema, mfumo huo utakuwa chachu ya ushiriki wa Diaspora wa Kitanzania kidigitali katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo biashara, uchumi na uwekezaji licha ya umbali waliopo.

“Kwa niaba ya uongozi wa Wizara na Serikali kwa ujumla natoa shukurani za dhati kwa uongozi mzima wa NSSF wa kukubali kushirikiana nasi katika jambo hili muhimu kwa kutoa Shilingi milioni 50,” alisema.

Aidha, Balozi Bwana amesema NSSF ni wadau muhimu wa kutoa huduma kwa Diaspora, ambapo pamoja na huduma hizo kupitia dirisha la uwekezaji, Wizara imekuwa na mazungumzo na NSSF ili kuangalia namna wanavyoweza kushirikiana zaidi katika eneo la Uwekezaji kupitia uendelezaji wa viwanja vilivyopo katika Balozi za Tanzania nje ya nchi.

Ameongeza kuwa, mfumo huo pia utawezesha kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali kuhamasisha taasisi mbalimbali nchini kuwekeza katika digitali ili kuongeza tija ya matumizi sahihi ya muda wanaohudumiwa na kupunguza urasimu, pamoja na kuiwezesha Wizara hiyo kwenda sambamba na dunia katika teknolojia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uthaminishaji, Takwimu na Usimamizi wa Hadhari Ibrahim Maftah akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, alisema Mfuko unatambua na kuthamini mchango wa Diaspora katika kujenga uchumi wa Taifa.

Maftah alisema, ushiriki wa NSSF katika kufanikisha kuanzishwa kwa mfumo huo unatokana na umuhimu wa suala lenyewe, lakini pia kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Diaspora wanachangia kikamilifu maendeleo ya uchumi wa Taifa.

“Wakati wote NSSF imekuwa moja ya wadau muhimu katika shughuli na matukio mbalimbali ya Diaspora, hivyo kupitia mfumo huo ni fursa kwa Mfuko kutangaza fursa mbalimbali za miradi ya uwekezaji kama vile nyumba, viwanja, hoteli na huduma nyingine zinazotolewa na NSSF,” alisema.

Hata hivyo, ameipongeza Wizara kwa kubuni wazo hilo la kuanzisha mfumo huo ambao utakuwa chachu ya mafanikio mbalimbali ya kuwaunganisha Watanzania waliopo nje ya nchi na fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Naye Mwakilishi wa Kitengo cha Diaspora Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Semeni Nandonde alisema kupitia mfumo huo Serikali itaweza kufahamu idadi ya Diaspora, ujuzi walionao, elimu pamoja na kupata huduma maalum ambazo zitaandaliwa kwa ajili yao kama vile huduma za hifadhi ya jamii, benki, bima ya afya, uwekezaji, biashara na masoko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live