Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NSSF haijapata wateja mradi wa Dege

FA2A09F5 FEEA 4F7A 992F AA71ED1FBEE6.jpeg NSSF haijapata wateja mradi wa Dege

Sun, 12 Feb 2023 Chanzo: Mwananchi

Ikitimia miezi mitano baada Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutangaza kuuza mradi wake wa Dege Eco Village uliogharimu Sh330 bilioni hadi sasa, hakuna mzabuni aliyefikia uwezo wa kununua mradi huo.

Mradi huo uliopo mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam ulioanzishwa na mfuko huo mwaka 2014 ukiwa na majengo ya hoteli, maduka makubwa, kumbi za mikutano, eneo la wazi la mapumziko, shule, nyumba za ibada, mighahawa, hospitali, baa na nyumba za kifahari ujenzi wake ulisimama tangu Januari 2016.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba alisema uamuzi wa kuuza mradi huo ulifikiwa kwa kuwa kulionekana kasoro katika tathmini ya awali kwani gharama zilizotakiwa kuukamilisha zilikuwa Sh1.5 trilioni ambazo ni nje ya uwezo wa mfuko wenyewe.

“Endapo itatokea hatujapata mtu ambaye atatupa bei ya kurudisha hiyo gharama, tutatoa nafasi ya kutangaza kwa mara nyingine hivyo ndivyo tulivyopanga ili kufikia lengo la kufidia zile fedha zilizotumika.

Kama itashindikana kabisa tutarudi kwa watoa uamuzi kuwapa hiyo taarifa,” alisema Mshomba. Akikazia suala hilo Mshomba alisema mradi huo utauzwa kwa mfumo wa kuwezesha kurudisha gharama zilizotumika ili kufidia gharama na angalau kubaki na faida.

Akizungumzia suala la NSSF kuuza mradi huo, mtaalamu wa masuala ya uchumi, Dk Paul Kapalango alisema ni hali ya kawaida kwa miradhi mikubvwa kuuzwa kwa wazabuni ila ni aibu kwa taasisi husika.

“Si jambo geni kuuzwa kwa miradi hasa kwa maslahi ya mfuko kama huo unaohudumia wananchi wanaojitafutia ila ni aibu na ni kuonyesha udhaifu hasa hapo kwenye kutathmini mradi kabla ya kuwekeza mabilioni ya fedha, inasikitisha,” alisema.

Kwa upande wa madeni wanayoidai Serikali, Mshomba alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ipo katika hatua ya kujiridhisha na madai ya madeni hayo ambayo hayazidi Sh500 milioni huku akidai mpaka Machi 2023 Serikali iteleza lini itawalipa madeni hayo.

Aidha mfuko huo umewalipa madeni ya Sh2.6 bilioni katika katika kipindi cha Juni hadi Disemba 2022 watumishi 183 waliofutiwa ajira kwa kukosa vyeti halali ambao walichangia kwenye mfuko kabla ya sheria ya uchangiaji kubadilishwa mwaka 2018.

Katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023, mfuko huo unatarajia kulipa mafao yenye thamani ya Sh769.3 bilioni ambayo ni ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na mafao ya Sh659.8 bilioni yaliyolipwa kipindi kama hicho mwaka jana.

Mtaalamu wa Biashara ya Nyumba kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Dk Sophia Kongela alisema mambo mengi yanasababisha hali kama hiyo kujitokeza kwa biashara ya miradi ya nyumba.

Ingawa alisema hajawahi kuuona mradi huo wa NSSF, kwa ujumla mambo yanayoweza kukwamisha miradi kama hiyo alisema ni ubora duni, eneo ulipo, gharama za kuukamilisha na lini utazalisha faida baada ya kuwekeza.

“Ili mwekezaji anunue mradi kama huo anaangalia kwanza ubora wake, lini mradi utamlipa iwapo ataununua na mara nyingi kwa Tanzania angalau uwe unamlipa ndani ya miaka 15 hadi 17 zaidi ya hapo ni changamoto kuuza,” alisema msomi huyo.

Dk Sophia aliyataja mambo mengine yanayoweza kuufanya mradi kuvutia kuwa ni eneo ulipo kwamba panatakiwa pawe panafikika, karibu na huduma muhimu.

“Pia mwekezaji anaangalia mradi umekaa kwa muda gani pengine kukaa kwake kumesababisha athari zozote ambazo akinunua atahitajika kufanya matengenezo na yatagharimu kiasi kikubwa cha fedha, haya yote yanaangaliwa na yanaweza kukukosesha wateja kulingana na fedha uliyotangaza,” alisema Dk Sophia.

Chanzo: Mwananchi