Benki ya NMB Plc imezindua kifurushi maalum cha mikopo yenye riba nafuu kwa walimu kuwawezesha kumudu gharama ya elimu kwa watoto wao, kujiendeleza kitaaluma, kununua vyombo vya usafiri na kulipia bima.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kifurushi hicho uliofanyika jijini Mwanza mwishoni mwa wiki, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi alisema kupitia kifurushi cha “Mwalimu Spesho” walimu nchini wataondokana na na adha ya mikopo ya mitaani yenye riba kubwa.
“Kupitia kifurushi cha Mwalimu Spesho, walimu watakopa kulipia gharama za elimu kwa watoto au kujiendeleza wenyewe kitaaluma kwa riba nafuu ya asilimia 10,” alisema Mponzi.
Kupitia kifurushi hicho, walimu pia watakopa kwa ajili ya shughuli za kilimo kwa riba ya asilimia tisa pamoja na kukopa kwa ajili ya kununua vyombo vya usafiri ikiwemo pikipiki na kulipia bima.
Kabla ya kupokea mikopo, Mponzi alisema walimu hao watapewa bure elimu ya fedha kuwaepusha na matumizi yasiyo ya lazima ili kuhakikisha mikopo hiyo inatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.
Akizundua kifurushi cha ‘Mwalimu Spesho” katika hafla iliyohudhuriwa na walimu zaidi ya 300 kutoka jijini Mwanza, Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Eng. Robert Gabriel aliipongeza benki ya NMB kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa walimu akisema itawakomboa kutoka kwenye mikopo ya riba kubwa inayotolewa na watu binafsi mitaani.
“Nawasihi walimu watumie vyema fursa ya mikopo kuanzisha miradi ya ujasirimali kujiongezea kipato bila kuathiri utendaji wala kuingilia muda wa kazi,” alisema Gabriel huku akizihimiza taasisi za fedha kuhakikisha zinatoa huduma jumuishi kwa wananchi wa kada zote hadi vijijini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Nyamagana, Sholi Maduhu na Mwalimu Grace Muyanja kutoka shule ya msingi Iseni walisema mikopo ya elimu, bima, kilimo na vyombo vya usafiri utaongeza ari ya kazi, ufanisi na utendaji wa walimu na hatimaye ubora kitaaluma na ufaulu wa wanafunzi.