Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NMB yawapoza wajasiriamali walioathirika na Covid-19

911aaa7589af4cdc628611ed2fec9ded NMB yawapoza wajasiriamali walioathirika na Covid-19

Thu, 12 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BENKI ya NMB imewatoa hofu wajasiriamali na wafanyabiashara wateja ikiwataka walioathirika na janga la virusi vya corona kuwasiliana na uongozi wa benki katika maeneo yao kujadili namna ya kukabili athari za kibiashara walizoipata kutokana na ugonjwa huo.

Meneja wa Benki ya NMB, Kanda ya Magharibi, Sospeter Magesse, alisema hayo katika kikao cha pamoja na wajasiriamali na wafanyabiashara wateja wa benki hiyo wilayani Kasulu kilicholenga kupeana taarifa na kuwekana sawa kuhusu suala zima la kusaidiana ili wafanyabiashara waendeshe shughuli zao kwa tija.

Magesse alisema kumekuwa na athari kubwa kwa wafanyabiashara baada ya kuingia janga la corona kwani biashara nyingi zilishuka na kuathirika hali iliyosababisha wafanyabiashara wengi kushindwa kurejesha mikopo yao huku wengine wakipoteza mitaji yao.

Alisema benki imefanya jitihada ya kukaa na wafanyabiashara hao kuona wanavyoweza kutibu majeraha yaliyotokana na janga hilo kwa pamoja.

Kuhusu kufanyika kwa mikutano hiyo, alisema kumekuwa na mafanikio makubwa kwa wafanyabiashara na benki kwani wamekuwa wakizungumzia mikakati ya kuimarisha biashara zao, kuongeza mikopo, namna ya kufanya marejesho na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza.

Alisema Klabu ya Wafanyabiashara wa NMB imekuwa ikitokea elimu ya uendeshaji biashara, utunzaji wa fedha na utafutaji masoko mambo aliyosema yamewezesha kuongezeka kwa uhusiano baina yao, kuongeza wateja wa benki na kuleta mabadiliko na mendeleo ya kibiashara kwa wafanyabiashara.

Mwenyekiti wa Klabu ya Wafanyabiashara wa NMB katika Wilaya ya Kasulu, Ephraem Mbweuka, alisema mikutano hiyo na elimu ya biashara inayotolewa imekuwa ikiwajenga wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa tija ikiwemo kuepuka hasara na kukabiliana na hasara biashara inapoyumba.

Mbweuka alisema pamoja na hilo, elimu ya matumizi ya mitandao na malipo ya fedha kwa njia ya kadi badala ya kutembea na fedha taslimu imekuwa na faida kubwa kwao katika kuepusha majanga ya kutapeliwa fedha zao.

Mfanyabiashara wa Wilaya ya Kasulu, Masudi Bigangika alisema wameathirika kwa kiasi kikubwa na janga la corona na kwamba vikao na wataalamu wa benki hiyo vimewatia faraja kuona namna ya kufanya marejesho bila kuathiri mtaji, lakini pia kupata mikopo ambayo itakayosaidia kurejesha biashara zao katika nafasi yake.

Chanzo: habarileo.co.tz