Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NMB yatoa vifaatiba kwa zahanati ya Mitwero

B5cded860f39d40b3b27e75add3819cb NMB yatoa vifaatiba kwa zahanati ya Mitwero

Sat, 6 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KATIKA kuhakikisha kwamba wadau wake wanakuwa na afya ya kutosha ili kuwawezesha kuzalisha zaidi na kuhifadhi pato lao benki, Benki ya NMB imetoa vifaa tiba kwa Zahanati ya Mitwero iliyopo wilayani Lindi, Mkoa wa Lindi vyenye thamani ya Sh milioni 5.

Vifaa tiba vilivyokabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga huku Mbunge wa Lindi mjini, Hamida Abdallah akishuhudia ni kitanda cha kujifungulia, vifaa vya kujifungulia , mashuka 20 na vitanda 3 vya wagonjwa .

Akipokea msaada huo Ndemanga, alishukuru na kusema msaada huo unachangia juhudi za serikali za kuhakikisha kwamba inapunguza vifo vya akina mama na watoto.

Aidha Mkuu huyo wa wilaya alisema kutokana na wadau kuendelea kuchangia vifaa tiba na uwingi wa watu eneo hilo kwa sasa wanahitaji ushirikiano wa kujenga kituo cha afya ili kuboresha huduma za afya katika eneo hilo linalotanuka kwa kasi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Huduma kwa Wateja wa Benki ya NMB Lindi, Eyya Ngolo alisema NMB wanaamini kuhusu afya na elimu kama msingi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa hivyo wanaporejesha faida kwa wananchi kwa mtindo huo wamelenga kutoa chachu zaidi kwenye shughuli za uchumi za wadau wake.

"Sisi ni benki inayojali maendeleo ya jamii na tunajua afya ndio msingi wa uzalishaji mali, kwa kutambua hili tunasaidia Afya na elimu" alisema Ngolo.

Alisema wao kwa miaka 10 wamekuwa wakirejesha asilimia 1 kwa wadau wao katika sekta ya elimu na afya na kwamba wenye mahitaji katika maeneo hiyo wanaweza kuwasiliana nao waone wanasaidia nini.

Pamoja na kupeleka vifaatiba katika zahanati hiyo inayohudumiwa wananchi zaidi ya 6,000 wakiwemo wanawake zaidi ya 3200 pia wanajipanga kupeleka misaada ya elimu kwa seondari ya Mitwero.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mitwero, David Lugomela pamoja na kuishukuru NMB kwa kuwasaidia vifaa tiba hivyo aliwaomba NMB na wadau wengine kusaidia kukarabati jengo la kujifungulia ambalo kwa sasa ni chakavu mno.

Alisema jengo hilo linahitaji Sh milioni 14 kubadili bati 30, milango na miundombinu mingine ili wanawake wengi zaidi waweze kujifungulia katika zahanati hiyo. Ingawa wanawake wanaojifungulia katika zahanati hiyo wameongezeka kutoka 15 mwaka juzi hadi 24 mwaka jana idadi ya wanaofika kliniki ni zaidi ya 157 lakini wengi wanakwenda hospitali ya mkoa kutokana na zahanati hiyo kuwa na ufinyu wa nafasi na vifaa.

Aidha waliomba kupatia huduma ya maji ambayo imekatwa kwa muda mrefu kutokana na limbikizo la deni na sasa wanategemea hisani kupata maji ya kuendeshea zahanati hiyo.

Akizungumza baada ya vifaatiba hivyo kukabidhiwa, Meneja wa NMB Lindi, Shaaban Kassari akizungumza kwa niaba ya Meneja wa NMB kanda ya Kusini Janeth Shango alisema wametoa vifaatiba ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za wadau wake wakubwa kukabili changamoto za jamii ili kuwepo na ukuaji mzuri wa kiuchumi kwa kusaidia sekta za afya na elimu.

Naye Mbunge wa Lindi, Hamida alisema kwamba amefarijika sana kupatikana vitanda hivyo ili kuondoa msongamano wa wanawake wanaokimbilia hospitali ya Mkoa ya Sokoine.

Wananchi waliohojiwa wakati wa makabidhiano hayo akiwamo Rukia Maulid, Asha Suleiman ma Selemani Simba walishukuru NMB kwa kuwakumbuka lakini wakaomba sana matengenezo ya jengo la kujifungulia kwa kuwa chumba kinachotumika kwa sasa hakina staha na pia kidogo. Aidha wametaka kusaidiwa upatikanaji wa maji na dawa ambazo zimekuwa adimu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz