Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NMB yatenga Bil 1.9/- ujenzi wa maghala

27e7e38d83761e04b0894be2492ccc66 NMB yatenga Bil 1.9/- ujenzi wa maghala

Mon, 3 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BENKI ya NMB mwaka huu imetenga Sh bilioni 1.9 zitakazotumika kujenga maghala ya kuhifadhia mazao eneo ambalo Serikali imesema linahitaji mchango wa taasisi za fedha nchini.

Benki hiyo imetenga kiasi hicho cha fedha kutimiza dhamira yake thabiti ya kuendeleza kilimo na kuwainua wakulima. Ufadhili huo mkubwa wa NMB uliwekwa wazi na Kaimu Ofisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo, Benedicto Baragomwa, alipokuwa anatoa maelezo kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alipotembelea banda la benki hiyo juzi kabla ya ufunguzi rasmi wa maonyesho ya Nane Nane.

Mkoa wa Simiyu umekuwa mwenyeji wa maonyesho hayo kitaifa tangu mwaka 2018 na Benki ya NMB imekuwa mmoja wa wafadhili wake wakubwa na mwaka huu imechangia Sh milioni 42.5 kuyafanikisha.

Katika maelezo yake pia, Baragomwa alimfahamisha Makamu wa Rais kuwa Benki ya NMB imeanza kusambaza na kuuza bima kwa wakulima kupitia huduma yake ya NMB Bancassurance . Ofisa huyo alisema huduma za bima ambazo mpaka sasa hivi zinatolewa na benki hiyo kwa wakulima ni pamoja na bima za hali ya hewa, bima ya mazao yalioko shambani, bima za moto na wizi (kwa mazao yaliyohifadhiwa) na bima kwa ajili ya vifaa vya kilimo.

Katika hotuba yake ya kuyafungua maonyesho hayo, Makamu wa Rais alisema Serikali tayari imeanzisha bima ya mazao itakayowafidia hasara watakayopata wakulima kutokana na ukame, uharibifu na uvamizi wa wadudu, mafuriko na majanga mengine.

Chanzo: habarileo.co.tz