Benki ya NMB imezindua mashine ya kwanza ya kutolea fedha (ATM) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), yenye uwezo wa kubadili fedha za kigeni kwenda shilingi za Kitazania.
Uzinduzi huo umefanyika jana Jumatatu Agosti 29, 2022 huku ikielezwa kuwa hiyo ni hatua nyingine muhimu kwa benki hiyo ya utoaji huduma kwa Watanzania wanaosafiri kutoka nje na watalii wanaoingia nchini.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alisema wateja na wasio wateja wa NMB sasa wanaweza kubadilisha fedha hadi Dola 2,000 za Marekani kwa wakati mmoja kwa viwango vya kubadilishia fedha vya NMB.
“Kiwango hiki ni zaidi ya Sh4.6 milioni za Kitanzania na kwa kuanzia, mashine hii itakuwa inauwezo wa kubadili Dola za Marekani, Euro za Umoja wa Ulaya na Pound ya Uingereza kwenda shilingi ya Tanzania,” alisema Zaipuna Mtendaji mkuu huyo alisema wameanza na aina hizo tatu za sarafu na muda si mrefu wataongeza fedha za mataifa mengine.
Hata hivyo, Zaipuna alisema uzinduzi huo ni muendelezo wa huduma hizo zilizozinduliwa kwa mara ya kwanza na taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.
“Tunatarajia pia kupeleka huduma hii kwenye maeneo mengine yakiwamo ya Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA), uwanja wa ndege Zanzibar na Zanzibar Stone Town.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alioupongeza uamuzi wa benki ya NMB kwa kuanzisha huduma hiyo aliyosema kuwa ilikuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu.
“Huduma hii ni faraja kubwa sana kwetu, tunapokea wageni wengi sana na wanauhitaji mkubwa sana wa kubadili fedha za kigeni hivyo, hili ni jambo jema sana kwa mkoa wetu,” alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Lakini alitoa wito kwa wale wote wanaosimamia huduma hizo KIA na wale wa benki ya NMB kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kama inavyotarajiwa na ziwe za kudumu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kadco ambao inaendesha shughuli katika uwanja wa KIA, Christina Makatobe alisema huduma hiyo ni muhimu kwa taasisi yao haswa ikitiliwa maanani kuwa hapo ni lango la kuingilia wasafiri wengi hasa watalii.
“KIA ni lango kuu la kuingilia wasafiri wengi wanaoingia hapa nchini haswa watalii na wafanyabiashara, kuweko kwa filamu ya Royal Tour Tanzania tunatarajia kupata watalii wengi zaidi siku za usoni hivyo huduma hii ni jibu kwa changamoto iliyokuwa ikiwakabili wasafiri wengi haswa wale waliokuwa wakiingia nyakati za usiku”, alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Ernest Ndunguru alisema uzinduzi wa ATM hizo kitakuwa kivutio cha watalii wengi nchini kutokana na ukweli kuwa huduma bora haswa za kifedha, ni moja ya vigezo ambavyo watalii hufuatilia kabla ya kutembelea nchi husika.