Wakati Benki ya NMB PLC ikijivunia faida ya mabilioni iliyoyapata mwaka huu, eneo lingine ambalo imefanya vizuri ni kukua kwa thamani ya mtaji wake katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) kwa karibu asilimia 50.
Kwa mwaka 2023, Benki ya NMB imetangaza kupata faida ya Sh542 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na kipindi kama hizo mwaka uliopita, jambo linaloifanya kuwa benki inayoongoza kwa faida hapa nchini.
Hata hivyo, mtaji wa NMB katika soko la DSE umeongezeka hadi Sh2.25 trilioni katika mwaka ulioishia Desemba 2023 kutoka Sh1.5 trilioni kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.
Kuongezeka kwa mtaji huo kunaifanya NMB kuwa benki kubwa zaidi kati ya zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa Tanzania na masoko yote ya hisa Afrika Mashariki.
Hayo yameelezwa leo Januari 30, 2024 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna wakati akitoa taarifa ya fedha ya benki hiyo katika mwaka 2023.