Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NMB yapata faida ya Sh569 bilioni

Fedhaa 0 NMB yapata faida ya Sh569 bilioni

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Benki ya NMB imetangaza kupata matokeo imara ya kifedha katika kipindi kilichoishia Septemba 30 mwaka 2023, ambapo faida kabla ya kodi ya Benki imefikia TZS Bilioni 569 ikiwa ni ongezeko la asilimia 23 ikilinganishwa na TZS Bilioni 464 za kipindi kama hicho mwaka jana. Faida baada ya kodi ya Benki hii kiongozi nchini imeongezeka kwa asilimia 22 na kufikia TZS Bilioni 398 ukilinganisha na TZS bilioni 324 zilizopatikana kipindi kilichoishia Septemba 2022.

Ufanisi huu mkubwa unaashiria mwendelezo wa utekelezaji makini wa Mkakati wa Benki na nidhamu kubwa ya utekelezaji wa Mkakati huo, ambapo matokeo yake ni ukuaji wa biashara, nidhamu yaudhibiti wa gharama za uendeshaji na usimamizi mzuri wa ukopeshaji. Ukuaji huu mkubwa wa biashara pia, ni matokeo ya utulivu na mazingira wezeshi ya kibiashara na kiutendaji nchini.

Benki imeendeleza ufanisi wa mapato ambapo mapato halisi ya riba yameongezeka kwa asilimia 20 hadi kufikia Bilioni 692, hasa kutokana na kuongezeka kwa mikopo kwa wateja binafsi na wale wakubwa.

Mapato yasiyotokana na riba nayo yameongezeka hadi kufikia TZS bilioni 334 ikilinganishwa na TZS bilioni 297 za mwaka 2022 ambalo ni ongezeko la asilimia 12. Ongezeko hili linatokana na wateja kutumia zaidi njia mbadala za huduma ambako kunaakisi matokeo chanya ya kasi ya uwekezaji katika masuluhisho ya kidijitali na bunifu ya kifedha.

Mizania ya Benki iliendeleza kasi ya ukuaji na kuvuka kiasi cha TZS trilioni 11.5 kufikia mwisho wa robo ya tatu ya mwaka 2023.

Ukuaji huu ulitokana na kuongezeka kwa mikopo na uwekezaji katika dhamana za Serikali.Mikopo halisi ilikuwa kwa asilimia 25 na kufikia TZS trilioni 7 mwishoni mwa robo hii ya mwaka, huku amana za wateja zikiongezeka kwa asilimia 15 hadi kufikia TZS trilioni 8.2.

Benki ya NMB inaendelea kuonyesha ufanisi mkubwa katika uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato, ambapo uwiano huu ulifikia asilimia 38 mwezi Septemba 2023 ukilinganisha na asilimia 41 kwa kipindi kilichoishia Septemba 2022.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live