Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NMB yapata faida bil 205/-

Ff2a8ae51b186752192019974314f930 NMB yapata faida bil 205/-

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BENKI ya NMB imetangaza kupata faida ya Sh bilioni 205.5 baada ya kodi kwa mwaka ulioishia Desemba 31, 2020 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 45.

Akizungumzia matokeo hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema yametokana na utendaji imara uliojielekeza kukuza mapato na kuongeza ufanisi kwa kutumia teknolojia na kupunguza gharama za uendeshaji.

“Kwa miaka mitano iliyopita, Taifa lilishuhudia ukuaji endelevu wa uchumi uliochangiwa na sera makini za fedha na kodi. Ni kutokana na mazingira haya wezeshi pamoaja na utekelezaji makini ya mpango mkakati wa benki tumefanikiwa kupata matokeo haya mazuri yaliyosaidia kukua kwa faida tuliyoipata,” alisema Zaipuna.

Faida ya benki kabla ya kodi iliongezeka kwa asilimia 40 kutoka Sh bilioni 211.1 iliyopatikana mwaka 2019 mpaka Sh bilioni 295.4 mwaka jana huku faida baada ya kodi nayo ikiongezeka kwa asilimia 45 kutoka Sh bilioni 142.2 mwaka 2019 hadi Sh bilioni 205.5 mwaka jana na kutifanya kuwa benki ya kwanza nchini kupata faida kubwa kiasi hicho.

Aidha, taarifa zake za fedha zisizokaguliwa pia zinaonesha faida hiyo imechangiwa na ongezeko la mapato ya biashara yaliyopanda kwa asilimia 15 na udhibiti wa gharama za uendeshaji ambazo ziliongezeka kwa asilimia mbili tu ndani ya mwaka huo.

Kutokana na mpango mkakati wa benki wa kuongeza ufanisi wa utendaji na huduma za kijiditali, mapato mengine yaliongezeka kwa asilimia 19 kutoka Sh bilioni 224 mwaka 2019 hadi Sh bilioni 266.2 mwaka jana yakichangiwa zaidi na ongezeko la wateja waliotumia huduma mtandaoni. Katika kipindi hicho, mapato yatokanayo na riba yaliongezeka kwa asilimia 11 kutoka Sh bilioni 518 za mwaka 2019 hadi Sh bilioni 574 mwaka jana.

Hata hivyo, tengo la mikopo chechefu liliongezeka kwa asilimia 19 kutoka Sh bilioni 100.4 mwaka 2019 hadi Sh bilioni 119.3 mwaka jana, mafanikio makubwa hasa ikizingatiwa changamoto kubwa iliyoletwa na janga la corona.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kama msimamizi wa sekta ya fedha ilitekeleza wajibu wake vizuri kwa kutoa mwongozo uliotoa nafuu ya ukwasi hata kurekebisha urejeshaji wa mikopo iliyotolewa kwa wateja hasa waliopo kwenye sekta zilizoathirika zaidi na janga la corona.

Kuthibitisha kwamba NMB ni benki inayochangia zaidi kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini, thamani ya mali zake iliongezeka kwa asilimia nane na kufika Sh trilioni 7.1 katika robo ya nne mwaka jana kutoka Sh trilioni 6.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2019.

Kupanda kwa thamani ya mali hizo kulitokana na ongezeko la amana za wateja kwa kiasi cha Sh bilioni 369. Mikopo iliyotolewa kwa wateja iliongezeka pia na kufika Sh trilioni 4.31 sawa na asilimia 15.

Aidha, mikopo hiyo iliongezeka kutoka Sh trilioni 3.76 zilizotolewa mwaka uliotangulia zikiwa ni juhudi za benki kukuza mikopo inayotoa kwa sekta binafsi. Kwa ujumla, amana za wateja zilipanda kwa asilimia saba kutoka Sh trilioni 4.9 mwaka 2019 mpaka Sh trilioni tano mwaka jana kudhihirisha imani waliyonayo wateja nchini juu ya NMB.

Ofisa Mtendaji Mkuu alisema mafanikio hayo yanatia moto na ni uthibitisho uwajibikaji wa wafanyakazi wa benki hiyo, utekelezaji na usimamizi wa mpango mkakati, kuungwa mkono na wadau tofauti pamoja na imani waliyonayo wananchi na wateja wengine sokoni.

“Tukiendelea kutekeleza na kusimamia mpango mkakati biashara wetu, benki imejielekeza katika kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji na matarajio ya wateja tukiongozwa na kuzielewa changamoto zao, huduma za kimtandao na uendeshaji wa shughuli zetu za ndani kidijitali zaidi ili kutufanya tuendelee kuwa juu wakati wote,” aliongeza.

Kwa mwaka jana, mafanikio ya Benki ya NMB yameifanya itambulike na kupata tuzo za kimataifa ikiwamo ya Benki Salama Zaidi Tanzania iliyotolewa na Jarida la Global Finance, na kunyakua tuzo ya Benki Bora Tanzania iliyotolewa na Jarida la Euromoney kwa mwaka wa nane mfululizo.

Ikihudumia takriban asilimia 22 ya wateja wote wanaotumia huduma za benki nchini na kupokea amana zao, NMB ndio yenye mizania mikubwa zaidi katika sekta ya fedha na inayoongoza kwa kupata faida kubwa nchini.

“Tunawashukuru wateja wetu, wafanyakazi, wanahisa, Serikali ya Tanzania, Benki Kuu pamoja na wabia wetu wa kimkakati kwa ushirikiano wanaoendelea kutupatia,” alisema Zaipuna.

NMB ni benki ya biashara iliyoanzishwa na kusajiliwa Tanzania ikiwa na matawi 225, zaidi ya mawakala 8,000 na zaidi ya mashine 800 za kutolea fedha (ATM) nchini na katika wilaya zote nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz