Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NMB kusaidia kufufua mkonge

4462ea1d5475d112a0cd5687739c92eb NMB kusaidia kufufua mkonge

Fri, 22 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

BENKI ya NMB imesema itahakikisha inaendelea kutoa huduma za kifedha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kampeni ya kufufua zao la mkonge na kuboresha uchumi wa wakulima wa zao hilo nchini ifanikiwe.

Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa kikao cha wadau wa mkonge kilichofanyika juzi mkoani Tanga, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa benki hiyo, Filbert Mponzi alisema waendeleza jitihada za kusaidia kufufua zao.

Alisema tangu serikali ilipoanza kulifufua zao hilo, benki hiyo imekuwa ikitoa ushirikiano ambapo imetoa zaidi ya Sh bilioni 1 kwa ajili ya ununuzi wa matrekta 11 na trela 22, vifaa ambavyo vitapunguza gharama ya uendeshaji na kuongeza tija na pato la wakulima wadogo wa mkonge.

Aidha, alisema benki hiyo imeendelea kutoa mikopo ya pembejeo na uendelezaji wa mashamba ya mkonge kwa wakulima wadogo, kati na wakubwa ili kuongeza uzalishaji na mapato ambapo zaidi ya Sh bilioni 6 zimeshatolewa kwa wakulima wa zao hilo.

Alisema NMB pia imefanikisha kufungua akaunti kwa wakulima zaidi ya 1,500 ambapo akaunti hizo zinajumuisha wakulima mmoja mmoja na wanaozalisha kupitia vyama vya msingi.

“Ili kuendelea kuwajengea uwezo wakulima wadogo na kupata mitaji, NMB kupitia taasisi tanzu ya NMB Foundation inaendelea kutoa mafunzo kwa wakulima kupitia vyama vya msingi na vikundi ili kuimarisha utendaji na kuongeza soko," alisema.

Akizungumza katika kikao hicho, Majaliwa alisema mpaka kufikia mwaka 2025 Tanzania inatarajia kuzalisha tani 120,000 za mkonge kwa mwaka.

Alisema zao hilo ni miongoni mwa mazao ya biashara hapa nchini ambayo mikakati yake ikitekelezwa vizuri itawezesha serikali kupata fedha nyingi za kigeni lakini pia kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema wizara hiyo imetenga Sh bilioni 175 kwa ajili ya kufanya utafiti ili kuzalisha mbegu bora na zenye gharama nafuu za mkonge.

Alisema wizara hiyo imeandaa utaratibu wa hati ya dhamana (LC) utakaowezesha wakulima wadogo kuchukua mkopo kwenye taasisi za fedha kwa riba ya asilimia mbili tu.

Chanzo: habarileo.co.tz