Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NMB kukopesha wananchi wapimiwe na kurasimisha ardhi

8767e13eeffbf1eacc5268ff615600c8.jpeg NMB kukopesha wananchi wapimiwe na kurasimisha ardhi

Thu, 12 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imezindua mpango wa kitaifa wa kuwakopesha wananchi fedha za kurasimishaji wa maeneo yao.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alizindua mpango huo jana katika Kata ya Igawa wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya na kueleza kuwa, mpango huo kwa nchi nzima na kwamba, Benki ya NMB itawakopesha wananchi fedha za kupanga, kupima na kuandaa hati.

Lukuvi alisema mpango huo umeanzia Mbarali kwa kuwamilikisha wananchi zaidi ya 52,000 kwa kuwa kazi nyingi za urasimishaji hazikufanikiwa kwa sababu baadhi ya wananchi walikosa fedha na kushindwa kulipia Sh 150,000 kwa mkupuo kugharimia upimaji na umilikishaji.

"Nimeamua kuanzisha mpango huu kwa kushirikiana na NMB ambao watawakopesha fedha za kupanga, kupima na kuandaa hati ambazo benki italipa asilimia 100 kwa mkupuo, kisha nyinyi mtalipa taratibu na kwa awamu kwa muda wa miezi 24 yaani miaka miwili," alisema.

Lukuvi alisema asilimia 90 ya wananchi wa Mbarali walikuwa hawakopesheki kwa sababu ya ardhi yao ilikuwa haijapangwa wala kupimwa.

"Baadhi ya wananchi wamekwamisha kazi hii ya urasimishaji katika maeneo mengi kwa kuwa wachache ndio wameweza kupata fedha za kugharamia upangaji, upimaji na umilikishaji kwa wakati.”

“Sasa NMB leo hapa Mbarali wamekuja kuwakopesha wananchi gharama zote. Na ninataka zoezi kama hili lifanyike nchi nzima na wengine waige kwa kufuata utaratibu huu," alisema.

Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa, aliwataka wananchi wachangamkie fursa hiyo ili kurasimisha maeneo yao.

Baragomwa alisema NMB itafanya kazi hiyo kwa kutumia matawi yote 226 nchi nzima.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo, aliwahakikishia wananchi kuwa, wizara hiyo itasimamia utekelezaji wa mpango huo na kwamba wananchi watapewa hatimiliki za ardhi za miaka 99 na watamilikishwa kisheria.

Chanzo: www.habarileo.co.tz