Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NIC yaridhishwa na Tanga Cement

3b83fe497efcf45be2f13feb9a8ab4ba NIC yaridhishwa na Tanga Cement

Sun, 25 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MENEJA wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Daudi Riganda leo ametembelea na kujionea shughuli za uzalishaji zinazofanywa na Kiwanda cha Saruji cha Tanga Cement kilichopo Jijini Tanga huku akieleza kuridhishwa na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na kampuni hiyo kwa kuchangia kukuza uchumi na maendeleo ya nchi.

Akizungumza mara baada ya kutembelea maeneo mbalimbali kwenye kiwanda hicho, Riganda alisema mwekezaji wa Kampuni ya Tanga Cement ni miongoni mwa wawekezaji mahiri waliosajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania na kupewa hadhi ya wawekezaji mahiri.

Alisema wamefika kiwandani hapo kuangalia uwekezaji uliofanyika na kuangalia mkataba “Performance Contract” uliosainiwa baina ya Serikali na Wawekezaji hawa ni namna gani ulivyotekelezwa na kila upande.

Katika ziara hii, TIC wamejionea uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 147.65 uliofanywa na kampuni hii, huku ajira zipatazo 330 za moja kwa moja na 677 zisizo za moja kwa moja zikitengenezwa kupitia uwekezaji huu. Kampuni ya Tanga Cement ni miongoni mwa makampuni yanayoongoza katika kulipa kodi katika Kanda ya Kaskazini.

Aidha Alisema imeonekana kwamba kuna matokeo makubwa yaliyopatikana upande wa teknolojia ambazo zimeingizwa nchini kupitia mradi huo huku akieleza kufurahishwa zaidi na namna kampuni hiyo ilivyofanikiwa kuajiri idadi ndogo ya wafanyakazi wa kigeni huku idadi kubwa ikiwa ni wafanyakazi wa Kitanzania, wengi wao wakiwa ni vijana wa kitanzania.

“Wapo wafanyakazi wa kigeni hawazidi watano na idadi kubwa walioajiriwa kwenye mradi huu wakiwa ni vijana wa Kitanzania kwa hakika hili limetufurahisha sana",alisema Meneja huyo

Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkazi Mtendaji wa Kiwanda cha Tanga Cement, Mhandisi Benedict Lema alisema kuwa kampuni ya Tanga Cement ilikuwa na mpango wa kufungua kiwanda kingine cha saruji mkoani Arusha jirani na eneo la uwanja wa ndege wa KIA, mradi ambao ulikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 50,hata hivyo wawekezaji hao wamesitisha mpango huo ambao ungetengeneza ajira na mapato zaidi kwa serikali, hadi hapo suala hili la kimkataba “performance contract” litakapopata suluhisho na kodi hiyo kusamehewa kama ilivyobainishwa kwenye mkataba.

Chanzo: www.habarileo.co.tz