Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

'NFRA lazima iwe kibiashara'

MGUMBAAA EDITED.webp 'NFRA lazima iwe kibiashara'

Mon, 4 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI imeweka bayana mpango mkakati wa kuhakikisha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) unajiendesha kibiashara na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, alibainisha mkakati huo jijini Dodoma mwishoni mwa wiki, alipofunga kikao kazi cha Bodi ya Ushauri ya NFRA.

Mgumba alisema serikali imetathmini mwenendo wa NFRA katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo na kujiridhisha kuwa umeanza kutekeleza majukumu yake ipasavyo, hivyo kuongezewa jukumu muhimu la kununua nafaka kwa ajili ya kuhifadhi chakula na kujiendesha kibiashara.

Aliutaka wakala huo kufanya ununuzi wa mazao kwa ajili ya kuhifadhi kama akiba kwenye maghala ya serikali, lakini kwa ajili ya biashara kwa kutafuta masoko ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri Mgumba alisema wakala huo una jukumu la kuhifadhi mazao ya kila aina na siyo kuchagua mazao ya kuhifadhi, akitolea mfano mahindi kuwa ndiyo yamekuwa yakipewa kipaumbele kulinganisha na mazao mengine.

Alisema serikali imetekeleza maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa, hivyo NFRA inapaswa kuhakikisha inanunua nafaka ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi na kufanya biashara.

Mgumba alisema NFRA inapaswa kununua mahindi, mpunga na mtama kwa kuwa mazao hayo ni fursa kutokana na uhitaji mkubwa wa chakula nchini na nje ya nchi.

"Unaweza kuwa na fedha nyingi, lakini kama huna mipango mizuri ya ununuzi, huwezi kupata mazao. Hivyo, NFRA ni lazima mjipange vizuri ikiwamo kuongeza vituo vya ununuzi.

"Msije mkanunua mahindi kisiasa, ni lazima mtenganishe siasa na biashara. Mkifanya hivyo, mtajichimbia shimo wenyewe, hivyo lazima mkafanye biashara kwa ajili ya kupata faida," aliagiza.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Yustas Kongolle, aliishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuwaamini yeye na wajumbe wa bodi hiyo kiasi cha kuwateua kuhudumu kwa miaka mitatu huku akisema watafanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa zaidi.

"Kuaminiwa na wizara maana yake nchi imetuamini, tunaahidi kufanya kazi kwa bidii na kutimiza maagizo yote ambayo tumeelekezwa kufanya ikiwa ni pamoja na kuifanya NFRA ijiendeshe kibiashara," aliahidi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Delphina Mamiro, ambaye ni Mjumbe wa Bodi hiyo ya NFRA, alisema bodi hiyo imejipanga kufanya kazi kubwa na nzuri zaidi.

Alisema mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa utakamilika hivi karibuni, hivyo kuna jukumu kubwa na muhimu la kuhakikisha utekelezaji wa ununuzi unakamilika kwa wakati.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live