Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NEMC yataka wanaopinga bomba la mafuta wapuuzwe

Bomba La Mafuta TANGA NEMC yataka wanaopinga bomba la mafuta wapuuzwe

Wed, 18 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limetoa ufafanuzi kuhusu mwenendo wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi rasi ya Chongoleani Tanzania (EACOP), likiwataka Watanzania kupuuza yanayosemwa na wanaharakati wa mazingira kuhusu mchakato huo.

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakidai kuwa utekelezaji wa mradi huo usababisha athari kimazingira zikiwemo uharibifu kwenye chanzo cha ziwa Victoria, bonde la mto Nile na utolewaji wa hewa chafu ya ukaa zaidi ya tani milioni 37 kwa mwaka.

Mbali na hilo, madai mengine ya wanaharakati hao kuhusu mradi huo ni pamoja na kuondolewa kwa makazi ya wananchi zaidi ya 1,000 ili kupisha ujenzi wa mradi huo, utakaogharimu dola 3.5bilioni za Marekani.

Lakini jana akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka aliwataka wananchi kupuuza yanayosemwa katika mitandao ya kijamii na wanaharakati wa mazingira hao kuhusu mradi, ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla.

“Wale ambao mnafuatilia mitandao ya kijamii puuzeni yale ambayo wanaharakati wanataka kuyaweka ili kuonekana ili bomba halina manufaa kwa Tanzania na Afrika Mashariki.Wananchi wote walioguswa na mradi huu, hali zao za maisha zitabadilika, kuliko walivyokuwa wakiishi awali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba bora za kuishi za kisasa,” alisema Dk Gwamaka.

“Hizi taarifa zimeanza mwaka jana na tulishuhudia wananchi wa nchi jirani wakipinga hili bomba na hivi karibuni tumeona katika mataifa ya Ulaya. Lakini kabla ya kukamilisha andiko la tathimin ya athari ya mazingira ya mradi kulikuwa na utaratibu rafiki wa kupeleka malalamiko au maoni kwa maandishi,” alisema.

Advertisement Mbali na hilo, kuanzia mwaka 2017 hadi 2019, Serikali ilitisha vikao mbalimbali ambavyo ingekuwa fursa kwa wanaharakati hao kutoa maoni, mapendekezo au malalamiko kuhusu mchakato wa mradi huo, badala ya kuupinga wakati utekelezaji wake umeshaanza.

Katika mkutano huo, Dk Gwamaka alieleza hatua kwa hatua ya namna Serikali ilivyoshiriki katika mchakato huo, ili kuhakikisha utaratibu na kanuni za uhifadhi na usimamizi wa mazingira unafuata katika utekelezaji wake.

Alisema kampuni ya Rsk Enviromental ya Uingereza ikishirikiana na wengine ni miongoni mwa kampuni za ushauri elekezi zilizotoa mwongozo kuhusu mradi huo. Katika mchakato huo NEMC ilihakiki andiko la tathimin ya athari ya mazingira kuhakikisha kwamba linazingitia na kuweka mipango inayothibiti

Mbali na hilo, Dk Gwamaka alisema taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, zilihusika katika kupata maoni yao kuhusu mradi huo.Timu ya NEMC na taasisi zinazohusika moja kwa moja na bomba hilo, walifanya ziara katika maeneo yote ya mradi huo kuanzia Februari 2 hadi 14 mwaka 2019.

“Mapitio ya tathimini ya athari kwa mazingira yalifanyika kwa awamu mbili; ya kwanza ilihusisha kikao cha kupata maoni ya wadau wote kuanzia ngazi ya kitaifa.

“Awamu ya pili ilikuwa kikao cha kamati ya ushauri wa kitaalamu kilichofanyika Aprili 3 mwaka 2019 kuhusisha watalaamu wa NEMC, vyuo vikuu, taasisi za Serikali na watalaamu elekezi na wawakilishi wa mradi huo,” alisema na kuongeza kuwa Novemba 29 mwaka 2019 Serikali ilidhinisha na kupatiwa cheti.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live