Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NEMC yaonya dizeli ya viwandani kuwekwa kwenye magari

44e4089c23ba85cd21bb1f90a53d5efb NEMC yaonya dizeli ya viwandani kuwekwa kwenye magari

Wed, 16 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeonya wamiliki wa vituo vya mafuta na wananchi kuepuka kununua dizeli inayozalishwa viwandani na kuitumia kwenye magari.

NEMC imetoa tahadhari hiyo, baada ya uwepo wa taarifa kuwa dizeli hiyo inayozalishwa kwa ajili ya kuendesha mitambo ya viwandani, inasambazwa katika baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta kwa ajili ya matumizi ya magari, jambo ambalo amesema linaweza kuwa hatari kwa usalama wa magari hayo.

Hatua hiyo imefuatia ukaguzi uliofanywa na Baraza hilo katika kiwanda cha kuchakata mafuta ghafi cha ‘Guoyang Biotech’ kilichopo Msongola wilayani Ilala, Dar es Salaam, baada ya kupokea taarifa kuwa dizeli inayozalishwa mahali hapo kwa ajili ya matumizi ya mitambo viwandani inasambazwa kwenye baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo kiwandani hapo, Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, amesema kimsingi mafuta hayo siyo salama kwa matumizi ya magari, kwani husababisha maisha ya injini ya gari kuwa ya kipindi kifupi.

Mkurugenzi huyo aliyeambatana na Kaimu Meneja kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Mashariki, Emmanuel Lewanga, amesema ni vyema wamiliki wa magari wakawa makini wakati huu, ambapo sampuli ya mafuta hayo imepelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Tulishituka tulipopata taarifa kuwa mafuta hayo yanasambazwa katika baadhi ya vituo kwa ajili ya matumizi ya magari na tukaona vyema kufika hapa kwa lengo la kujiridhisha ili pamoja na mambo mengine pia tuone kama taratibu zetu za mazingira zinazofuatwa mahali hapa,” amesema Dk Gwamaka.

Kwa upande wake, Lewanga amesema wamechukua sampuli ya mafuta hayo na kwenda kuyapima ili kujua aina ya kemikali inachanganywa na baadae watatoa ripoti na kuikabidhi NEMC kwa ajili ya hatua zinazofuata

Chanzo: www.habarileo.co.tz