Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NDC yatafuta mwekezaji kuzalisha matairi 900,000

8c6a8bd152916d508bdcf6ad6f77a598 NDC yatafuta mwekezaji kuzalisha matairi 900,000

Fri, 16 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHIRIKA la Maendeleo la Taifa (NDC) linatafuta mwekezaji mzoefu na mwenye uwezo washirikiane kujenga kiwanda cha kisasa cha matairi jijini Arusha.

Kwa mujibu wa tangazo la Mkurugenzi Mtendaji NDC, kiwanda hicho kitakachojengwa na kampuni ya pamoja kitakuwa na uwezo wa kuzalisha matairi 900,000 kwa mwaka.

Katika tangazo hilo, NDC ilieleza inahitaji mwekezaji anayetengeneza aina ya matairi yanayotambulika duniani ili ishirikiane naye kwa niaba ya serikali waanzishe kiwanda kipya cha kisasa.

“Kiwanda kipya cha kutengeneza matairi kitaendeshwa na kampuni ya pamoja itakayoundwa na NDC na mwekezaji,” alieleza Mkurugenzi Mtendaji NDC.

Alisema kiwanda hicho kitazalisha aina mbalimbali za matairi na kwamba, mwekezaji mwenye nia ya kushirikiana na NDC anapaswa kutoa taarifa kuthibitisha ana sifa zinazohitajika za kiufundi, watumishi, kifedha na usimamizi.

Uongozi wa NDC kupitia tangazo kwenye gazeti la serikali ulieleza kuwa, serikali imelipa shirika hilo mamlaka ya kuhamasisha ukuaji wa viwanda vya msingi nchini.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, NDC pia imepewa mamlaka ya kuanzisha na kuwezesha maendeleo ya miundombinu ya viwanda vya kisasa kwa ajili ya maendeleo endelevu ya sekta hiyo.

Lilieleza kuwa, kiwanda cha awali cha matairi Arusha cha General Tyre East Africa Limited kilikuwa na uwezo wa kuzalisha matairi 320,000 kwa mwaka lakini kilisitisha uzalishaji mwaka 2009 kwa sababu ya ukosefu wa rasilimali fedha.

Kwa mujibu wa tangazo la NDC, kiwanda hicho kilichopo Njiro ni cha kizamani, teknolojia yake imepitwa na wakati na hakiwezi tena kumudu ushindani kwenye soko la dunia.

“Kutokana na hilo serikali iliipa NDC jukumu la kujenga kiwanda kipya na cha kisasa cha kutengeneza matairi kwenye eneo hilo hilo mkoani Arusha kwa kushirikiana na mwekezaji,” ilieleza.

Chanzo: www.habarileo.co.tz