Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NBS yauchambua mfumuko wa bei

45681 Pic+nbs NBS yauchambua mfumuko wa bei

Sun, 10 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS) imesema bei za bidhaa zisizo za chakula zimeongezeka kwa Februari 2019 ikilinganishwa na bei za Februari 2018 ikiwa ni pamoja na gharama za kumuona daktari katika hospitali binafsi kuongezeka kwa asilimia 4.6.

Akizungumza leo Ijumaa Machi 8, 2019, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Jamii wa NBS, Ephraim Kwesigabo ametaja bei zilizoongezeka katika kipindi hicho pia kuwa ni mavazi, ongezeko la asilimia 2.7, mkaa kwa asilimia 10.1 na majokofu kwa asilimia 2.1.

Amesema hata hivyo mfumuko wa bei katika kipindi cha mwaka unaoishia Februari 2019 umebakia kuwa asilimia 3.0 kama ilivyokuwa kwa mwaka unaoishia Januari 2019.

"Hii inamaanisha kasi ya mabadiliko ya bei ya bidhaa na huduma kwa mwaka unaoishia Februari 2019 imebaki sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka unaoishia Januari 2019," amesema.

Amesema hali hiyo imechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za chakula kwa kipindi kinachoishia Februari 2019 zikilinganishwa na Februari 2018.

Ametaja mfano wa baadhi ya bidhaa kuwa ni mchele asilimia 3.0, unga wa mahindi kwa asilimia 6.4, mtama asilimia 5.1, unga wa mihogo kwa asilimia 6.9, maharage kwa asilimia asilimia 4.5 na viazi vitamu kwa asilimia 8.2.

Kwesigabo amesema mfumuko wa bei kwa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Februari 2019 umepungua hadi asilimia 0.5 kutoka asilimia 2.7 kwa mwaka unaoishia Januari 2019.

Akilinganisha na mfumuko wa bei katika nchi za Afrika Mashariki, amesema nchini Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Februari 2019 umeongezeka hadi asilimia 3.0 kutoka asilimia 2.7 kwa mwaka ulioishia Januari 2019.

Amesema kwa upande wa Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Februari 2019 umepungua kidogo hadi asilimia 4.14 kutoka asilimia 4.70 kwa mwaka ulioishia Januari 2019.



Chanzo: mwananchi.co.tz