Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NBS yataja sababu za kutotumika kwa takwimu

Nbs Takwimu.png NBS yataja sababu za kutotumika kwa takwimu

Thu, 21 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema asilimia 40 ya takwimu zinazotokana vyanzo visivyozoeleka zinashindwa kutumika kwa sababu hazina uhakika wa ubora wake.

Akifunga mafunzo ya watakwimu yaliyoandaliwa na Chuo cha Takwimu Afrika Mashariki (EASTC) leo Alhamisi Machi 21,2024, jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu, Utafiti na Shughuli za Kitakwimu wa NBS, Emilian Karugendo amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuendeleza Takwimu awamu ya pili (TSNP).

Amesema awamu ya kwanza ilijikita katika miundo msingi lakini awamu ya pili imejikita katika uimarishaji wa vyanzo vingine vya takwimu ukiacha tafiti na sensa.

Karugendo amesema takwimu wanazozalisha kupitia vyanzo vya asili yaani tafiti na sensa zinachangia sio zaidi ya asilimia 60 ya zinazohitajika kuripoti maendeleo au utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

“Zaidi ya asilimia 40 ya takwimu tulizonazo zinatoka katika vyanzo visivyozoeleka kwa maana kuna changamoto ya takwimu ambazo zinatokana na vyanzo ambavyo havijazoeleka vya takwimu za kiutawala,”amesema.

Amesema takwimu za kiutawala ni zile zinazopatikana kutokana na utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya utendaji na kuwa zipo nyingi katika halmashauri nchini.

Karugendo amesema taarifa hizo zimekuwa hazitumiki kwa sababu hawana uhakika na ubora wake kwa maana ya ukamilifu wa taarifa.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Mipango, Fedha na Utawala wa EASTC, Dk France Shayo amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa wataalamu wa takwimu kutoka halmashauri na manispaa zote.

“Mpango huu tumeanza kuutekeleza kwa kuwa na wahudhuriaji 50 kutoka mikoa saba ambao tumekuwa nao kwa siku 10 na kesho tutakuwa na wataalamu 60 kutoka mikoa saba kwa ajili ya mafunzo hayo,”amesema Shayo.

Amesema jumla ya watakwimu 220 kutoka katika mikoa mbalimbali wamejifunza matumizi ya kompuyuta kwa kukusanya, kuchakata na kuhifadhi taarifa kupitia mfumo wa Excel.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Mtakwimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Mkoa wa Dodoma, Hilda Fodi amesema mafunzo hayo yamewasaidia kupata ujuzi wa jinsi ya kutengeneza takwimu zitakazotumika katika sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya uamuzi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live