Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NBS yaonya wazalishaji nyaya za umeme

D4ec6cc67dc492ed88ee2dff65886231.jpeg NBS yaonya wazalishaji nyaya za umeme

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji wa nyaya za umeme nchini kuacha kuzalisha nyaya zililokatazwa matumizi yake kote duniani ili kuendana na matakwa ya soko la kimataifa.

Akizungumza hivi karibuni mkoani Dar es Salaam, Ofisa viwango wa TBS, Henry Massawe alisema kwa mujibu wa matakwa hayo ya soko la kimataifa la bidhaa hiyo, nyaya zenye rangi nyeusi na nyekundu hazipaswi kuwepo sokoni na badala yake zitumike nyaya zenye rangi ya bluu na kahawia.

Alisema cha kushangaza pamoja na uwepo wa makubaliano hayo ambayo baadaye walikubaliana na wenye viwanda ili kuyatekeleza, bado kumekuwepo baadhi ya wenye viwanda hivyo kukiuka, jambo alilosisitiza kuwa ni ukiukwaji wa makusudi wa makubaliano hayo.

“Tunawataka wenye viwanda hivyo ambavyo bado vinazalisha nyaya hizo pamoja na waagizaji wa nyaya kutoka nje ya nchi kuzingatia kile tulichoagiza na kuanzia sasa tutapita maeneo yote kufanya ukaguzi ili kuona nani anakiuka,” alisema Massawe.

Alisema lengo la TBS ni kuhakikisha bidhaa bora na zenye viwango ndizo pekee zinazoendelea kuwepo sokoni, hivyo watafuatilia ili kuwabaini wale wanaoendelea kuzalisha au kuagiza nyaya hizo na kuingiza nchini kinyume cha utaratibu.

Hatua hiyo ya TBS imekuja siku chache baada ya baadhi ya wafanyabiashara, mafundi wa umeme pamoja na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kulitaka shirika hilo kutoa ufafanuzi wa nyaya zinazopaswa kuwepo katika soko ili kuwaondolea mkanganyiko wa matumizi wa nyaya hizo.

Wafanyabiashara pamoja na wananchi hao, walisema kwa namna hali ilivyo sasa ni ngumu kwao wao kutambua nyaya zipi hususani za uunganishaji wa umeme majumbani zinapaswa kuwepo madukani na nyaya zipi hazitakiwi kuwepo.

Mmoja wa wafanyabiashara hao kutoka Kariakoo, Alfan Idrissa alisema cha ajabu licha ya agizo hilo kutolewa, bado nyaya hizo zenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na nyekundu zimeendelea kuuzwa, jambo aliloomba lifuatiliwe.

Chanzo: www.habarileo.co.tz