Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NBS yafafanua kupanda bei za nyanya, vitunguu

95329 Vyakukla+pc NBS yafafanua kupanda bei za nyanya, vitunguu

Tue, 11 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/ mikoani. Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema mfumuko wa bei nchini hadi Januari 2020 ni asilimia 3.7 ukiwa umeshuka kwa asilimia 0.1 kutoka 3.8 kwa Desemba 2019.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Ruth Minja akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, amesema bei za vyakula hazijapanda kama inavyoelezwa na kuwa, inatarajia kushuka zaidi kutokana na maeneo mengi ambayo hivi sasa yanajiandaa kuingia katika msimu wa mavuno.

Taarifa hii ya NBS imekuja wakati bei za bidhaa za vyakula katika mikoa mbalimbali nchini zikiendelea kupanda na kusababisha kilio cha hali ngumu kutawala katika kipindi hiki cha mwanzoni mwa mwaka 2020. Bidhaa kama za nyanya, vitunguu na mkaa, bei yake imepanda mara dufu.

Hata hivyo, Minja alisema bidhaa hizo hazina athari katika mfumuko wa bei.

Alisema katika kupima mfumuko wa bei nchini, bidhaa kama nyanya haiwezi kuwa kigezo cha bei kuwa juu au chini kwa kuwa haina madhara kwenye mfumuko. “Ni kweli nyanya ziko juu pamoja na vitunguu, lakini athari yake katika mfumuko wa bei siyo kubwa ukilinganisha na vyakula kama vingekuwa vimepanda,” alisema Minja.

Akizungumza kuhusu kupungua kwa mfumuko wa bei, Mtakwimu huyo alisema katika mwaka unaoishia Januari 2020, kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi za vyakula zikilinganishwa na Januari 2019.

Pia Soma

Advertisement
Amezitaja baadhi ya bidhaa za vyakula zilizopungua ni dagaa kwa asilimia 1.4, viazi (3.4), magimbi (7.1) na ndizi za kupikwa zilizopungua kwa asilimia 2.8.

Kuhusu bidhaa zisizo za chakula, alitaja kuwa ni mafuta ya taa yalipungua kwa asilimia 4.6, petroli (1.5) na dizeli (1.3).

Majiko ya gesi (4.6) pamoja na gesi ambayo imekuwa ikilalamikiwa lakini wanasema imepungua kwa asilimia 2.0.

Alisema katika kipindi hicho, mfumuko wa bidhaa na vinywaji baridi ulipungua hadi asilimia 5.7 kutoka asilimia 6.3 kwa mwaka ulioishia Desemba 2019.

Ofisa huyo amezungumzia mfumuko wa bei kwa nchi ya Kenya kwa mwaka ulioishia Januari 2020 nako umepungua hadi asilimia 5.78 kutoka asilimia 5.82 wakati Uganda umepungua hadi kufikia asilimia 3.4 ukitoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia Desemba 2019.

Hapa nchini, taarifa toka mikoa mbalimbali zinaeleza kuwa bei za nyanya na vitunguu zimepanda maradufu hatua ambayo inaelezwa kusababishwa na kuharibika kwa miundombinu kutokana na mvua zinazoendelea na mazao hayo kusombwa na mafuriko.

Lakini pia, wataalamu wa kilimo wanasema kipindi hiki cha mvua si msimu wa mazao hayo. “Nyanya na vitunguu huwa hazihimili mvua na huu si msimu wake ndiyo maana zimepungua kwa kiwango kikubwa sokoni,” amesema Jerome Haule, mtaalamu wa kilimo.

Mwananchi lilitembelea baadhi ya masoko nchini na kukutana na malalamiko ya wafanyabiashara na wanunuzi wakilalamikia bidhaa hizo kupanda bei.

Sado ya nyanya ambayo ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh3,000 hadi Sh7,000, sasa inauzwa Sh14,000 huku vitunguu vikifika Sh4,000 kwa kilo kutoka Sh800 hadi Sh1,500 huku fungu la nyanya likiuzwa kwa Sh1,000.

Bei ya mchele jijini Mwanza imepanda kutoka Sh1,800 kwa mchele supa hadi kufikia Sh2,500 kwa kilo moja, mchele wa kawaida umepanda kutoka Sh1,500 kufikia Sh2,100, bei ambayo haitofautiani sana na mikoa ya Dar es Salaam na Arusha ambako unauzwa kwa Sh1,800 hadi Sh2,500 hadi jana mchana.

Upande wa unga katika jiji la Dar es Salaam unauzwa kwa Sh1,800 kwa kilo sawa na Mwanza wakati Arusha ukiuzwa kati ya Sh1,400 hadi Sh1,600.

Karanga jijini Mwanza zimeonekana kuongoza kwa kuwa na bei kubwa ya Sh3,000 kwa kilo moja kutoka Sh2,000.

Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro kreti la nyanya limepanda bei kutoka Sh45,000 hadi Sh85,000 kwa sasa huku vitunguu vikipanda hadi Sh240,000 kutoka Sh170,000.

Mfanyabiashara wa soko hilo ambaye anajihusisha na biashara ya mafuta ya kula, George Sizia alisema mafuta ya kula aina ya Safi yamepanda bei kutoka Sh28,500 kwa lita 10 hadi Sh33,000 kutokana na mafuta hayo kununuliwa kwa dola.

Chanzo: mwananchi.co.tz