Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NBC yatambulisha mikopo kwa wajasiriamali isiyo ya dhamana

National Bank Of Commerce Building In Dar Es Salaam 2012 NBC yatambulisha mikopo kwa wajasiriamali isiyo ya dhamana

Thu, 9 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BENKI ya NBC imetambulisha mikopo isiyo na dhamana kwa wajasiriamali wadogo na wa kati nchini, lengo ni kuwasaidia waweze kukua kibiashara.

Kadhalika, lengo ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kufanikisha uchumi wa viwanda.

Akizungumza kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara wa benki hiyo, Elvis Ndunguru, alisema mikopo hiyo inawalenga wajasiriamali wenye zabuni za kampuni kubwa.

“NBC tumechukua hatua hii ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo na wa kati kwa kutambua kwamba kwa kuwawezesha ndio tutakuwa tunaisaidia pia serikali kufanikisha agenda yake ya uchumi wa viwanda,” alisema.

Hatua ya benki hiyo inakuja huku tafiti zikionyesha wajasiriamali wadogo na wa kati wanashikilia asilimia 95 ya biashara zote nchini na ni moja ya sekta zinazokua kwa kasi zaidi kiuchumi, huku ikichangia asilimia 35 ya Pato la Taifa (GDP).

"Hivyo basi, NBC tumeona kuna umuhimu wa kukua sambamba na sekta hii ambapo tumekuwa tukifanya tafiti mbalimbali za kimasoko ili kutoa huduma sahihi za kifedha zinazozingatia mahitaji yao kuelekea mafanikio ya ukuaji wa kiuchumi,” alisema.

Alisema benki hiyo ilitoa mafunzo sambamba na kutoa mikopo yenye thamani zaidi ya Sh. bilioni 80 kwa wajasiriamali takribani 3,000 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita pekee, huku akibainisha kuwa benki hiyo inatarajia kutoa mikopo zaidi.

Alizitaja sekta ambazo zimenufaika na mikopo hiyo ni za biashara, makandarasi, mafuta na gesi, utalii na hoteli, usafirishaji, viwanda na kilimo.

Kwa mujibu wa Ndunguru, benki hiyo inafanya mikakati mbalimbali ikiwamo kuipitia upya sera yake ya mikopo kwa wajasiriamali sambamba na kuunda kamati mpya ya mikopo ya biashara ili kuleta usawa katika kufanya maamuzi.

"Zaidi NBC tunatarajia kuondoa sharti linalowataka wajasiriamali kuandaa taarifa za kifedha pale wanapoomba mikopo iliyo chini ya Sh. milioni 100,” alisema na kuongeza:

"Lengo haswa ni kuurahisisha mchakato wa mikopo na nyaraka zinazohitajika kutoka kwa wajasiriamali ili kuufanya mfumo uwe rahisi zaidi hatimaye kurahisisha ukuaji wa uchumi.”

Alisema benki inapanga kuelimisha na kukaribisha vilabu vya biashara kwenye hafla mbalimbali pamoja na maonyesho ya kibiashara ili kuwawezesha wajasiriamali hao kukutana na wenzao wakubwa na wawekezaji kutoka nje.

Aliongeza kuwa benki hiyo imeanzisha mpango wa wajasiriamali ikilenga kujiimarisha zaidi katika soko linalohusu sekta hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live