Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NBC yaipeleka mashine ya miamala Mlima Kilimanjaro

Mt Kilimanjaro 1110x700 NBC yaipeleka mashine ya miamala Mlima Kilimanjaro

Sun, 17 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Moshi. Wafanyakazi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na wadau mbalimbali wa utalii mkoani Kilimanjaro wameanza safari ya kihistoria ya kupanda mlima kwa lengo la kufikisha mashine ya kufanyia miamala ya benki hiyo kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Hatua hiyo mbali na kusogeza huduma za benki hiyo kwa wateja wake wanaotembelea mlima huo, pia inalenga kudhihirisha umahiri wa teknolojia ya NBC katika utoaji wa huduma zake kwa wateja.

Hafla ya kuiaga timu ya wafanyakazi hao wanaotarajiwa kushuka mlima huo Desemba 21, mwaka huu, imefanyika leo Jumapili Desemba 17, 2023 katika lango la Marangu, ikiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wateja wadogo na Binafsi wa NBC, Elibariki Masuke na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Angela Nyaki.

Akizungumza wakati akikabadhi mashine hiyo kwa timu ya wapanda mlima hao, Masuke amesema jitihada hizo ni mwendelezo wa kampeni mpya ya ‘Tabasamu Tukupe Mashavu’ inayolenga kutoa fursa kwa wateja kufurahia sikukuu za mwisho wa mwaka kupitia miamala iliyorahishwa kupitia benki hiyo.

“Tuko hapa kushuhudia historia mpya katika mapinduzi ya huduma za kibenki kupitia kampeni yetu ya ‘Tabasamu Tukupe Mashavu’ ambayo haijawahi kujaribiwa awali, yaani huduma ya kwanza kabisa ya mashine ya malipo juu ya Mlima Kilimanjaro,” amesema Masuke.

Amesema kampeni hiyo ni zaidi ya safari ya kupanda mlima kwa dhana ya kimwili bali ni kielelezo cha kujitolea kwao katika utambuzi na matumizi ya kidijitali katika utoaji huduma kwa wateja wao.

Amesema vituo sita kuelekea kwenye kilele cha Mlima huo mrefu barani Afrika, kwao havimaanishi tu hatua za upandaji bali pia ni vituo sita vya sifa ya kipekee vya mashine hiyo POS ambayo amesema huduma zake ni ishara ya maendeleo.

“Kila kituo kinatoa fursa kwa timu ya wafanyakazi wetu na wadau wetu wote wanaoshiriki safari hii, kushiriki historia tajiri ya mlima wetu huu tunaojivunia kama hazina yetu ya kitaifa na historia ya ukuu na urithi wetu,” amesema Masuke.

Amesema wakiwa kileleni, timu hiyo itafungua pazia la kuruhusu mashine hiyo kuanza kutoa huduma ya miamala kwa wateja kwa njia mbalimbali za malipo ya kidijitali kwa kadi ya aina yoyote ya benki.

Akizungumza hatua ya benki hiyo, Kamishna Msaidizi Nyaki licha ya kuipongeza NBC, amesema huduma hiyo itarahisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wadau wanaotembelea mlima huo.

“NBC mnapeleka kifaa hiki si tu kwenye kilele kirefu Afrika bali pia duniani. Niwapongeze sana kwa kuona umuhimu wa kutambulisha huduma hii duniani kupitia hifadhi hii mashuhuri. Mashine hii itasaidia wadau wa utalii kufanya miamala huko huko juu…tunashukuru sana kwa hatua hii,” amesema Nyaki.

Amewapongeza pia wadau wa habari mkoani Kilimanjaro kwa kuendelea kuhabarisha umma kuhusu upatikanaji wa mtandandao wa mawasiliano kwenye Mlima Kilimanjaro, hatua ambayo imeendelea kuwavutia watu mbalimbali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live