Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzabuni stempu za kielektroniki ajibu hoja tatu

10498 Pic+stemp TanzaniaWeb

Mon, 2 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya mjadala mkubwa kuibuka bungeni kuhusu uendeshaji wa mradi wa stempu za kodi za kielektroniki (ETS), kampuni ya Sicpa, ambayo ilishinda zabuni hiyo, imetoa ufafanuzi wa hoja tatu za kuipinga.

Sicpa itaendesha mradi huo wa kuweka stempu za kielektroniki katika eneo ambalo bidhaa zinazalishwa, lakini Kamati ya Bajeti na baadhi ya wabunge walipinga wakisema mradi huo utaongeza gharama kwa wazalishaji na kupandisha bei, wengine wakidai utamnufaisha zaidi muwekezaji badala ya Serikali na wengine kudai unaifanya Serikali iweke rehani uhuru wa nchi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Ghasia alisema wajumbe wamejiridhisha kuwa kampuni hiyo ya Uswisi itakuwa inakusanya zaidi ya Sh66.69 bilioni kutoka kwenye maji, sigara, jusi na bia kwa mwaka kiasi ambacho ni kikubwa kuliko uwekezaji utakaofanywa.

Lakini Ghasia alisema kampuni hiyo inatarajiwa kuwekeza dola 21.53 milioni za Kimarekani ambazo ni sawa na Sh48.5 bilioni.

Alishauri Serikali iwekeze katika mradi huo ili fedha zitakazokusanywa zitumike kwa shughuli za maendeleo badala ya kuchukuliwa na mwekezaji. Hoja hiyo ilidakwa na wabunge kadhaa waliopendekeza Shirika la Simu (TTCL) lipewe zabuni hiyo na baadaye Rais John Magufuli akasema kuwa mzabuni hataweza kufanya kazi zaidi ya miaka miwili.

Sicpa yajibu

Lakini jana Sicpa ilitoa ufafanuzi wa hoja hizo katika barua pepe kwenda kwa gazeti hili.

Hoja ya kwanza ya Sicpa ni takwimu za fedha zitakazowekezwa na zile zitakazokuwa zinapatikana kila mwaka ndani ya miaka mitano ya mkataba.

Imesema Sh48.5 bilioni zinazoelezwa kuwa ndizo zitakazowekezwa ni makadirio ya chini sana na kwamba kwa mahitaji yaliyopo yatazidi kiasi hicho hata kile kinachotarajiwa kukusanywa.

Katika baruapepe hiyo, mkurugenzi wa uhusiano wa Sicpa, Christine Macqueen alisema baada ya tathmini, gharama za uwekezaji zimeongezeka mara tatu zaidi.

“Napenda umma ufahamu gharama za uwekezaji zilizosemwa na Kamati ya Bunge ni makadirio ya chini sana, ikilinganishwa na uwekezaji wa awali uliofanywa na Sicpa,” alisema Christine.

Alisema kiasi kilichotajwa hakikuzingatia gharama za uendeshaji wa kila siku zinazohitajika kuufanikisha mradi huo.

Kuhusu mapato, alisema: “Yatakuwa yanabadilika kulingana na kiasi cha bidhaa zinazozalishwa. Hakuna uhakika sana kwenye eneo hili, lakini makadirio yetu yanaonyesha kiasi kitakachopatikana huenda kikawa theluthi moja ya yanayosemwa (Sh66.69 bilioni).”

Kuhusu kuweka rehani uhuru kutokana na mradi huo wa mawasiliano ya kielektoriniki kuendeshwa na kampuni ya nje, Sicpa imesema haitauendesha badala yake itaukabidhi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao watakaokuwa na mamlaka.

Christine alisema taarifa na mfumo mzima utakabidhiwa TRA kwa ajili ya uendeshaji.

“Ingawa baadhi ya vifaa vitakodishwa, mfumo mzima pamoja na taarifa zitakazokusanywa, zitakuwa chini ya uangalizi wa mamlaka za Serikali ya Tanzania na utaendeshwa kwa viwango vya TRA,” alisema mkurugenzi huyo.

Kampuni hiyo imesema mjadala kuhusu stempu hizo ulikuwa mkubwa, hivyo imelazimika kufafanua takwimu zinazohusu mradi huo ambazo alisema huenda hazikueleweka kwa wadau muhimu wa maendeleo ya Taifa.

Hoja ya Kamati ya Bajeti iligusa baadhi ya wabunge, na hasa mmoja wa wenyeviti wa chombo hicho cha kutunga sheria, Mussa Hassan Zungu.

Zungu, ambaye ni mbunge wa Ilala (CCM) alisema wakati akichangia hoja hiyo iliyokuwemo kwenye hotuba ya bajeti ya Serikali ambayo ilisomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philp Mpango, kuwa kuipa nafasi kampuni hiyo kukusanya kodi ni kuuza uhuru wa Tanzania kusimamia mambo yake.

Zungu alitahadharisha kuwa kampuni hiyo ina kashfa za kukiuka sheria kwenye baadhi ya nchi inakotekeleza baadhi ya miradi yake, ukiwemo kama huo wa stempu za kielektroniki.

Lakini, katika uchambuzi wake wa bajeti ya Serikali, chama cha ACT Wazalendo kilisema mpango huo ni mzuri, lakini upatikanaji wa mzabuni haukuwa wa wazi kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“Serikali itangaze upya zabuni ya mradi huo kwenye vyombo vya habari vya ndani na kimataifa ili kampuni tofauti zishindane,” ilisema ACT Wazalendo.

Katika moja ya kurasa zake za tovuti, Sicpa inajinadi kuwa suala la ukubwa wa gharama si kitu kikubwa kulinganisha na uidhibiti wa ubora wa bidhaa na ukwepaji kodi.

Chanzo: mwananchi.co.tz