Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwijage: Umaskini unasababisha kuzagaa bidhaa feki sokoni

18182 Pic+mwijage TanzaniaWeb

Wed, 19 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema uwepo wa bidhaa hafifu na feki sokoni ni kutokana na watumiaji wenyewe kuzihitaji kwa kuwa hawana nguvu ya kununua bidhaa bora.

Mwijage amesema hayo leo Septemba 19 katika uzinduzi wa semina ya Jukwaa la Ushindani la Afrika (ACF), unaofanyika jijini hapa kujadili namna ya kufanya uchunguzi na kudhibiti hujuma sokoni.

“Uwepo wa bidhaa bandia unatokana na umaskini wa watu, hawana nguvu ya manunuzi, ndiyo maana wanakimbilia bidhaa bandia ili kupata unafuu wa bei, kama Serikali tutaendelea kupambana na bidhaa hizo, lakini mapambano ya kweli ni kupambana na umaskini,” amesema Mwijage.

Amesema watu wote wanapenda nguo nzuri, magari mazuri na bidhaa bora kwa ujumla lakini hawana uwezo wa kununua na wazalishaji wa bidhaa hafifu na bandia wana uhakika wa kuuza bidhaa zao kwa kuwa soko lipo.

Kuhusu semina hiyo Mwijage amesema kwa asilimia kubwa hujuma hufanywa na kampuni kubwa zenye uwezo wa kutawala soko lakini hapa nchini hakuna magwiji kama hao na Serikali ina nguvu ya udhibiti wa soko.

"Hujuma hufanywa na kampuni kubwa za uzalishaji au usambazaji wa huduma muhimu kwa watu, hapa kwetu hazipo bado Serikali ina nguvu ya udhibiti wa bidhaa hizo, mfano bei ya mafuta inadhibitiwa na Ewura, tuna MSD kwa ajili ya kudhibiti mfumko wa bei za dawa, kwa ufupi sisi hatuna tishio hilo," amesema Mwijage.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) Dk John Mduma ambao ndiyo wenyeji wa semina hiyo amesema kwao kukutana na wenzao ni fursa adhimu kwani wataweza kubadilishana ujuzi kuhusu namna ya kushughulika na kampuni zinazofanya njama sokoni.

"Kuna hujuma za kampuni kufanya njama katika usambazaji au bei kwa maslahi yao binafsi, yanaweza kufanya hivyo lakini yasiwepo hapa nchini tukishirikiana na wenzetu ni rahisi kushughulika nayo," amesema Dk Mduma.

Chanzo: mwananchi.co.tz