Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwigulu avutia wawekezaji nchini Uingereza

Mwigulu Avutia Wawekezaji Nchini Uingereza Mwigulu avutia wawekezaji nchini Uingereza

Wed, 22 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa wito kwa wafanyabiashara na kampuni kubwa za nchini Uingereza kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo za uendelezaji miundombinu, nishati na kilimo ambazo zitachangia kukuza uchumi wa nchi na kuongeza upatikanaji wa ajira kwa vijana.

Dkt. Nchemba ametoa wito huo mjini London nchini Uingereza alipokutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara na wawekezaji katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Royal Africa Society.

Alisema kuwa amani na usalama vilivyopo nchini, upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kuwekeza, uwepo wa idadi kubwa ya walaji likiwemo soko la ndani na soko la ukanda, linalokadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni 400, ni fursa nyingine itakayowawezesha wawekezaji hao kupata faida katika uwekezaji wao.

Dkt. Nchemba alisema kuwa hivi sasa, biashara kati ya Tanzania na Uingereza imezidi kukua mabapo kiwango cha bidhaa ambacho Tanzania inasafirisha kwenda Uingereza kimefikia thamani ya shilingi bilioni 34.9 kwa mwaka nakiwango cha bidhaa kinachoingizwa Tanzania kutoka Uingereza kimefikia wastani wa shilingi bilioni 309 kwa mwaka.

Dkt. Nchemba aliwahakikishia wawekezaji hao tarajiwa, kwamba Serikali itaendelea kuboresha sera za uwekezaji na kuwatoa hofu kwamba Serikali ina sera za uwekezaji za uhakika, za kuvutia na zinazotabirika ili iweze kushiriki kikamilifu katika biashara za kimataifa, kikanda na kukidhi soko la ndani.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na MIpango-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, amesema kuwa mkutano huo umekuwa na manufaa ambapo idadi kubwa ya wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki mkutano huo wameonesha nia kuwekeza katika sekta mbalimbali za Zanzibar ikiwemo katika mkakati wa kukuza uchumi kupitia uchumi wa buluu.

Wakizungumza katika kikao hicho, wawekezaji hao walipongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuhamasisha uwekezaji pamoja na kuweka mazingira mazuri na rafiki ya uwekezaji na ufanyaji biashara.

Mkurugenzi wa Shirika la Royal Africa Society, Dkt. Nicholas Westcott, alisema Tanzania imejaaliwa kila aina ya fursa ambazo wawekezaji kutoka Uingereza wameonesha nia ya kwenda kuwekeza nchini humo.

Wawekezaji hao watarajiwa, walipongeza hatua za Serikali za kuweka mazingira tulivu ya uchumi pamoja na uwepo wa Sera nzuri zinazovutia uwekezaji na kwamba watakwenda Tanzania kujionea zaidi fursa hizo na kuwekeza teknolojia na mitaji, pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Dkt. Nchemba anaongoza ujumbe wa Tanzania nchini Uingereza ambapo anafanya mikutano na wadau mbalimbali na kueleza hatua ambazo nchi imefikia kiuchumi na katika ujenzi wa miundombinu itakayosaidia kuchochea kazi ya maendeleo ya nchi pamoja na kuomba uungwaji mkono wa jitihada hizo za Serikali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live