Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwigulu ataja mbinu kukabili kupanda gharama

C68980300725bc8a7aaaab5c532fffa5.PNG Mwigulu ataja mbinu kukabili kupanda gharama

Wed, 16 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema serikali imekuwa ikichukua hatua kukabiliana na kupanda bei kwa baadhi ya bidhaa ambazo pia zinapandisha gharama za maisha ambako hakutokani na sera za ndani, uzembe au uamuzi wa serikali, bali majanga yanayoikumba dunia.

Akielezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani mwaka jana, Dk Mwigulu alitaja majanga hayo kuwa makubwa ni janga la Covid-19 na sasa vita baina ya Urusi na Ukraine.

Baadhi ya bidhaa ambazo zimepanda bei kutokana na majanga hayo alizitaja kuwa ni zinazoagizwa nje kama ngano, mafuta ya kupikia, mbolea, mafuta ya mitambo na magari na vifaa vya ujenzi.

Hata hivyo, alisema serikali imekuwa ikijitahidi kupambana na mfumuko wa bei na ndio maana umetoka asilimia 4.0 hadi sasa ni asilimia 3.7.

“Kunapotokea majanga kama haya, waungwana hawanyoosheani vidole bali kupambana na hali ilivyo pamoja na kumwomba Mungu alete ahueni,” alisema Dk Mwigulu.

Akitoa mfano, alisema bei ya ngano kabla ya Machi 2019, yaani kabla ya Covid-19, kilo 100 zilikuwa zinauzwa Sh 100,000 za Tanzania.

“Lakini ilipoingia Covid na kisha vita vya Urusi na Ukraine sasa kiwango hicho ni shilingi 140,000. Hapo ni bei ya kulekule inakotoka kabla ya kusafirishwa hadi bandarini na sekta binafsi na kisha isafirishwe hadi tuseme Kigoma,” alisema.

Mafuta ya kupikia ya asili ya mawese alisema kabla ya Covid-19 bei ilikuwa chini ya Sh 3,000 kwa lita kule yanakonunuliwa mafuta, lakini baada ya Covid-19 yalipanda hadi zaidi ya Sh 5,600. Kwa upande wa mbolea, alisema aina ya BAP kabla ya Covid, gunia la kilo 50 lilikuwa Sh 57,000 kwa bei ya juu, lakini baada ya Covid imefikia Sh 110,000 kabla haijafikishwa nchini.

Mbolea ya Urea ilikuwa Sh 52,000, lakini sasa ni Sh 104,000. Kwa upande wa mafuta ghafi ya mitambo bei ilikuwa Sh 140,000 lakini sasa baada ya Covid ni Sh 267,000. “Petroli ilikuwa shilingi 1,158,000 ikapanda kidogo baada ya Covid hadi kwenye shilingi 1,500,000 lakini kwa tani ni shilingi 2,5000,000.

Dizeli ilikuwa shilingi 1,200,000, ikaenda shilingi 1,400,000 baada ya Covid-19 na sasa kufuatia vita ni shilingi 2,500,000. Mafuta ya taa yalikuwa shilingi 1,200,000, ikapanda hadi shilingi 1,400,000 lakini sasa baada ya mapigano ni shilingi 2,400,000,” alisema.

Alisema vifaa vya ujenzi kama bati, nondo na chuma bei yake pia zimeongezeka maradufu.

Alisema kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mafuta, hata bei ya mafuta ya ndani kama alizeti imepanda kutoka wastani wa Sh 4,000 kwa dumu la lita tano kabla ya Covid hadi kufikia wastani wa Sh 35,000 sasa.

Hata hivyo, alisema serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kupambana na majanga haya ya kidunia na hatua hizi ni kuzidi kufungua uchumi ili kuzalisha kwa wingi.

Alisema ni wakati wa Watanzania kupambana ili wasitoke kwenye reli na ndio maana bajeti ijayo itajikita zaidi katika kupanua kilimo, hasa cha umwagiliaji.

Hata hivyo, alisema kuna wanaopandisha bei za vitu hata walivyoagiza nje kabla ya kupanda kwa bei, hao wanadhibitiwa.

Kadhalika alisema katika bajeti ijayo, wamepata maelekezo kutoka kwa Rais Samia ili kuangalia namna ya kurekebisha kodi ili kupunguza makali ya gharama ya bidhaa hizo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live