Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwigulu: Uchumi umeongezeka kwa kasi

41577c3422cb6c6a14c08c8082780562 Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha

Wed, 8 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Fedha na Mipango imesema imepata mafanikio mengi katika mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa kasi ya ukuaji uchumi na kuwezesha mfumuko wa bei kubaki ndani ya matarajio ya wigo wa nchi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema jana bungeni Dodoma kuwa katika mwaka huo uchumi wa taifa ulikua kwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Mwigulu alisema hayo wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Alisema ongezeko la ukuaji wa uchumi limetokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na wizara ikiwamo kuwezesha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kurejea katika hali ya kawaida baada ya kuathirika na Covid-19.

Alisema kati ya Julai 2021 hadi Aprili mwaka huu mfumuko wa bei ulikuwa wa wastani wa asilimia 3.9 ikilinganishwa na asilimia 3.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2020/2021.

“Pamoja na ongezeko hilo, kiwango hicho bado kipo ndani ya matarajio ya wigo wa nchi wa kati ya asilimia tatu hadi tano na lengo la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki la asilimia nane,” alisema.

Alisema hadi Aprili mwaka huu, ukusanyaji wa mapato ya serikali umefikia Sh trilioni 19.99, sawa na asilimia 93.3 ya makadirio ya kukusanya Sh trilioni 21.42 katika kipindi hicho.

Kati ya kiasi hicho, mapato ya kodi yamefikia Sh trilioni 17.20, sawa na asilimia 94.5 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 18.2.

Aidha, wizara imewezesha wizara, idara zinazojitegemea, wakala na taasisi za serikali kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya jumla ya Sh trilioni 2.03, sawa na asilimia 81.2 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 2.5.

Alisema mamlaka za serikali za mitaa zilikusanya Sh bilioni 759, ikiwa ni asilimia 104.8 ya lengo la kukusanya Sh bilioni 724.1 katika kipindi hicho.

Dk Mwigulu alisema hadi Aprili mwaka huu wizara ilifanikisha upatikanaji wa mikopo ya Sh trilioni 4.12 kutoka soko la fedha la ndani.

Kati ya kiasi hicho, Sh trilioni 2.63 zimegharimia mikopo ya ndani iliyoiva na Sh trilioni 1.49 zimegharimia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katika kipindi hicho, wizara imefanikisha upatikanaji wa mikopo ya jumla ya Sh trilioni 1.81 kutoka katika masoko ya nje yenye masharti ya kibiashara.

Mwigulu alitaja mafanikio mengine kuwa ni kukamilisha maandalizi ya nyaraka za mapitio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, kuandaa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2022/2023 uliowasilishwa bungeni Machi mwaka huu na baadaye utawasilishwa tena katika bunge Juni mwaka huu.

Alisema wizara hiyo pia imefanya uchambuzi wa maombi ya fedha kwa miradi ya kimkakati 38 kutoka halmashauri 28 yenye thamani ya Sh bilioni 288.06.

Wizara pia imefanya ufuatiliaji na tathmini ya ujenzi wa madarasa 15,000 na mabweni 50 yaliyojengwa chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya athari za kiuchumi na kijamii za Covid-19.

Pia imefuatilia na kutathmini mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa Standard Gauge (SGR), mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo– Busisi na barabara unganishi, Kampuni ya Ndege (ATCL) na mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere Megawati 2,115.

Vilevile wizara imefuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi 173 ya maendeleo katika sekta za kilimo, viwanda, utawala bora, ujenzi, uchukuzi, maji, elimu, afya, biashara na mifugo katika mikoa ya Tabora, Kigoma, Geita, Kagera, Mara na Simiyu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live