Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka watanzania kutumia benki kuhifadhi fedha zao ili kuhakikisha usalama wa fedha zao na usalama wao na kuacha tabia ya kuhifadhi fedha majumbani.
Waziri Dkt. Nchemba aliyasema hayo jijini Dodoma wakati akizundua Tawi la Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo na kushindwa kutokana na majukumu mengine ya Kitaifa.
Dkt. Nchemba alisema ni vema wananchi wakajenga utamaduni wa kutumia benki kwa kuwa uendeshaji wa uchumi wa kisasa unategemea zaidi matuminzi ya utaratibu wa kibenki ambao kwa sasa umerahisishwa na unapatikana kwa urahisi.
Aidha, Dkt. Nchemba amesema Serikali kupitia Wizara ya Fedha itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na benki zote hapa nchini kama utekelezaji wa sera jumuishi za masuala ya kifedha na kiuchumi zinazolenga kuwasogezea wananchi huduma karibu hasa hizi za kifedha.