Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Mhe. Jerry Silaa ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa kuamua kutekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la abiria katika kiwanja cha Ndege cha Mpanda.
Akizungumza Mkoani Mpanda, Mwenyekiti Mhe. Silaa amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutaongeza idadi ya ndege na abiria na hivyo kukuza pato la mkoa na kuchagiza biashara baina ya Mkoa huo na mikoa mingine pamoja na nchi jirani ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Serikali imefanya jambo kubwa sana mkoani hapa hasa ukizingatia ujenzi wa bandari ya Karema umekamilika na mipango ya Serikali ni kujenga reli ya Kisasa, na hapa kuna ujenzi wa jengo la abiria umeanza vyote hivi vitafungua sana mkoa huu, natoa pongezi kwa Serikali’ amesema Mwenyekiti Silaa.
Mwenyekiti Mhe. Silaa amesema ni wakati muafaka sasa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kukitangaza Kiwanja hicho ili kuvutia mashirika mengi zaidi kwani kwa sasa kuna ndege ya Serikali tu inayotoa huduma kwa ratiba.
Mwenyekiti Silaa ametumia fursa hiyo kuitaka TAA kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana mradi wa jengo utakapokamilika ili kulifanya kukaa muda mrefu bila kuomba tena fedha za ukarabati.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Viwanja vya Mikoa kutoka TAA, Hamisi Amiri amesema ujenzi wa jengo hilo unatekelezwa na Kampuni ya Wesons Engineering Limited na litagharimu takriani shilingi bilioni 1.4 na litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 240 kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi Amiri ameongeza kuwa pamoja na mradi huo kuna mradi mwingine utakaotekelezwa unaohusisha ujenzi wa barabara ya usalama kiwanjani utakaogharimu takribani shilingi milioni 149 na miradi yote miwili inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.
Aidha, Mkurugenzi Amiri amemuhakikisha Mwenyekiti huyo kuwa Mamlaka imejipanga kumsimamia Wakandarasi hao ili wakamilishe mradi huo kwa wakati na viwango vilivyokubalika.
Kamati ya Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), iko Mkoani Mpanda kwa ziara ya siku mbili ambapo imepokea taarifa na kukagua miradi inayotekelezwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.