Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwelekeo wa bajeti kuu ulivyo kicheko wizara 14, panga lapita wizara saba

BAJETI+BUNGENI+PIC TZW

Thu, 7 Jun 2018 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati bajeti kuu ya mwaka wa fedha 2018/19 ikitarajia kusomwa bungeni Juni 14, wizara 14 zimekuwa na kicheko baada ya kupata nyongeza kwenye bajeti zao zilizopendekeza huku nyingine saba zikipigwa panga.

Kwa ulinganifu na kiasi kilichopitishwa katika bajeti ya 2017/18, jumla ya Sh1.48 trilioni zimeongeka katika wizara zote 14, ikiwa ni ongezeko la wastani wa asilimia sita kwa kila wizara imeongezeka katika bajeti ya 2018/19 kufikia Sh26 trilioni. Hata hivyo, upembuzi uliofanywa na Mwananchi umeonyesha wizara iliyopata nyongeza kubwa ya fedha ni Wizara ya Nishati ambayo bajeti yake imeongezeka kwa asilimia 78.9.

Fedha za wizara hiyo zimeongezeka kutoka Sh945.89 bilioni katika bajeti ya 2017/18 hadi Sh1.69 trilioni katika bajeti iliyosomwa ya 2018/19, ikiwa ni ongezeko la Sh746.11 bilioni. Wizara ya Nishati inafuatiwa na ya Ufugaji na Uvuvi iliyopata ongezeko la asilimia 58.6 la Sh20 bilioni. Ongezeko lake ni kutoka Sh35.6 bilioni katika bajeti ya 2017/18 mpaka Sh56.45 bilioni bajeti ya 2018/19. Ongezeko kwa wizara 12 nyingine zilizobaki lilikuwa ni chini ya asilimia 50.

Wizara hizo ni pamoja na Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (asilimia 18.2) kwa nyongeza ya Sh5.13 bilioni, huku Viwanda, Biashara na Uwekezaji ikiongezwa kwa asilimia 17.3 kwa kupata nyongeza ya Sh21.13 bilioni na Kilimo asilimia 13.32 kwa nyongeza ya Sh20.02 bilioni. Kwa ile ya Maji na Umwagiliaji ni kwa asilimia 13 ikiwa ni nyongeza ya Sh83.63 bilioni. Kwa wizara nyingine kama Madini ni asilimia 12.4, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki asilimia 12 na Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni asilimia 11.8.

Zilizobaki ni zile ambazo ongezeko lao ni chini ya wastani wa jumla wa asilimia sita ambazo ni Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (asilimia 3.3), Elimu, Sayansi na Teknolojia (asilimia 2.9), Fedha na Mipango (asilimia 2.6), Mambo ya Ndani (asilimia 1.6) na Tamisemi (asilimia 0.2). Kwa upande mwingine, wizara saba zimepigwa panga kwa wastani wa asilimia 9.23 kwa kila mojawapo.

Mwananchi limebaini kuwa jumla ya fedha kwa wizara zote saba zimepungua kutoka Sh6.94 trilioni mwaka 2017/18 hadi kufikia Sh6.3 trilioni kwa mwaka 2018/19, ikiwa ni upungufu wa takriban Sh641.31 bilioni. Hata hivyo, Wizara ya Maliasili na Utalii inaongoza kwa kupunguziwa kiasi kikubwa cha fedha kwenye bajeti yake ambayo imepungua kwa asilimia 22.28, ambayo ni zaidi ya mara mbili ya wastani wa asilimia 9.23 ambao ndiyo jumla ya punguzo kwa wizara zote saba.

Bajeti ya Maliasili

Bajeti ya Maliasili na Utalii imepungua kwa Sh33.21 bilioni na kufikia Sh115.79 bilioni kwa mwaka wa fedha 2018/19 kutoka Sh149 bilioni iliyotengwa katika bajeti ya 2017/18. Wizara hiyo imefuatiwa na Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kwa kupunguziwa asilimia 16 pamoja na ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (asilimia 10.5) ambazo zimepigwa panga la Sh171.7 bilioni na Sh78.79 bilioni kila moja.

Bajeti ya Wizara ya Afya imefyekwa mpaka kufikia Sh898.3 bilioni kutoka Sh1.07 trilioni za bajeti iliyopo, huku Utawala Bora ikibaki na Sh669.09 bilioni kutoka Sh747.88 bilioni. Pia Wizara ya Katiba na Sheria imefyekwa asilimia 15 ikipata punguzo la Sh24.89 bilioni kutoka Sh166.47 bilioni katika bajeti iliyopo hadi Sh141.58 bilioni katika bajeti ya 2018/19.

Wizara nyingine ni ile ya Waziri Mkuu (asilimia 11.1) ikiwa ni punguzo la Sh32.5 bilioni; Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (asilimia 6.2) ikipunguziwa Sh300 bilioni na ya mwisho ni Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira (asilimia 1.5) ambayo imepigwa panga la

Sh0.22 bilioni. Wizara ya Fedha na Mipango ndiyo imekula kiasi kikubwa cha bajeti nzima kwa kupewa fedha nyingi na kuchukua zaidi ya asilimia 37.2 ya bajeti nzima.

Wizara hiyo imepata kiasi cha Sh12.06 trilioni kati ya Sh32.4 trilioni inayokadiriwa kama bajeti kuu. Wizara hiyo imefuatiwa na Tamisemi iliyomega asilimia 20 ya bajeti yote ikiwa imepitishiwa kiasi cha Sh6.58 trilioni. Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeshika nafasi ya tatu kwa kuchukua asilimia 13 ya fedha zote zitakazotengwa ikiwa inatarajia kupewa Sh4.2

trilioni.

Ukiacha wizara zilizochukua asilimia kubwa kuna baadhi zimechukua chini ya asilimia moja ambazo ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge (0.80), Katiba na Sheria (0.4), Muungano na Mazingira (0.04), Viwanda, Biashara na Uwekezaji (0.44).

Maoni ya wachumi

Wataalamu na wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaeleza kuwa faida na hasara za kuongeza na kupunguza fedha kwenye wizara tofauti wametofautiana kimtazamo. nyingi kwenye miundombinu na kuacha wizara ambazo zinagusa maisha ya watu moja kwa moja. Mkurugenzi wa Utafiti wa Repoa, Abel Kinyondo anasema ni vyema Serikali kuweka fedha nyingi katika wizara ambazo zinawagusa watu moja kwa moja kama Kilimo, Afya na Elimu.

“Kwa mfano kupunguza bajeti ya Afya kwa asilimia 16 na ongezeko dogo kwenye Elimu kunaweza kuleta matokeo hasi ya rasilimali watu huko mbeleni,” alisema. Kwa upande wake, mchumi na mtaalamu wa biashara, Dk Donath Olomi anasema katika kila fedha iliyotengwa kwenye wizara iboreshe mazingira ya utendaji, huku zikipunguza matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija na ufanisi kulingana na kiasi walichopata. “Haijalishi bajeti ni ndogo au ni kubwa, ikiwa itatumika kuboresha utendaji katika kukidhi mahitaji ya watu kupata bidhaa na huduma zinazohitajika ninaamini uchumi wetu utaendelea kuimarika,” anasema.

Kwa nini punguzo la bajeti?

Mchumi, Profesa Delphin Rwegasira wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema kupunguza kiasi cha fedha kwenye baadhi ya wizara ni kiashiria kwamba Serikali imegundua kuwa bajeti zilizopita zilikuwa hazina uhalisia. Profesa Rwegasira anapongeza uamuzi wa Serikali kwa kuwa bajeti ya sasa itakuwa inayoweza kutekelezeka kutokana na rasilimali zilizopo nchini. “Kuwa bajeti tunayoweza kuimudu kwa rasilimali zilizopo ni bora zaidi maana tutapunguza kutegemea mikopo kutoka nje na kufanya hivyo kutapunguza deni la Taifa lililopo,” anasema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live