Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwekezaji mpya mwendokasi kutua wiki ijayo

Mwendokasi Pc Data Mwekezaji mpya mwendokasi kutua wiki ijayo

Mon, 31 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Wakati njia ya Mbagala ikitarajiwa kuwa na mabasi 750 yatakayosafirisha kati ya abiria 600,000 mpaka 700,000 kwa siku, awamu ya kwanza ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (Udart), imepata mwekezaji mwingine atakayeboresha huduma katika njia iliyopo sasa hivi.

Kampuni hiyo mpya ya Emirates National Group kutoka Falme za Kiarabu itaingia mkataba na Wakala wa Mabasi Yaendayo haraka (Dart) wiki ijayo, ili kuanza kutoa huduma ikiingiza mabasi mapya 177 yatakayosaidiana na yaliyopo tangu kuzinduliwa kwa mradi huo mwaka 2016.

Tovuti ya kampuni hiyo iliyoanzishwa mwaka 1990 inaonyesha imekuwa ikijishughulisha na kukodisha magari na utoaji wa huduma za usafiri wa umma na binafsi, huku makao makuu yake yapo Abu Dhabi, Falme za Kiarabu.

Ujio wa mabasi hayo 177, Dart imesema kutaongeza uwezo wa kuwahudumia abiria kutoka 200,000 wa sasa hadi abiria 500,000 wanaohudumiwa kila siku na usafiri huo ambao kwa miezi ya hivi karibuni umekuwa ukisuasua kutokana na uchache wa mabasi unaosababisha abiria kukaa vituo kwa muda mrefu.

Juzi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usafirishaji wa Dart, Fanuel Karugendo alisema baada ya kutangazwa kwa zabuni, kampuni hiyo ya Kiarabu iliibuka mshindi baada ya kukidhi vigezo vyote.

Ikumbukwe mwendeshaji wa kwanza Udart alikuwa katika majaribio ya mradi huo kwa awamu ya kwanza na kumekuwepo na danadana za muda mrefu za kampata mzabuni mpya kwa takribani miaka mitano sasa.

Akifafanua zaidi hilo, Karugendo alisema mchakato wa kumpata mzabuni huyo ulikuwa wa wazi kupitia Ushirika wa Serikali na Sekta Binafsi (PPP) na baada ya kusaini mkataba huo wiki ijayo atapewa miezi sita kuyaingiza mabasi hayo nchini.

“Ni uamuzi wake, anaweza kuyaleta nusu baada ya kumaliza kusaini mkataba na mengine kuyamalizia ndani ya miezi sita ilimradi tu asivuke muda kama mkataba unavyotaka,” alisema Karugendo.

Utaratibu wa matumizi ya kadi kulipia usafiri huo alisema unarejea baada ya mashine ya majaribio kituo cha Morocco kuwa na ufanisi.

“Majaribio yalifanywa na wataalamu wetu kwa kushirikiana na wataalamu wa mifumo kutoka Colombia na baada ya mwendeshaji mpya kuanza kazi, abiria sasa watatumia kadi, sio tiketi tena. Mfumo huo mpya wa kielektroniki wa kukusanya nauli umetengenezwa na wataalamu wazawa na hivi sasa ndio unatumika kukatia tiketi wakati huu tunaendelea kuleta kadi,” alisema Karugendo.

Shukuru Othuman, mkazi wa jijini hapa alisema wamepata adha ya kutosha, hivyo ujio wa kampuni hiyo unaweza kuboresha huduma.

Eva Thomas naye alisema “tunaomba Mungu mabasi hayo yafike salama, nina imani mambo yatakuwa safi katika huduma.”

Kwa upande wake, Ashura Ngaiza alisema ni “matarajio yangu huduma itakuwa ya kutukuka kuliko ilivyo sasa ambapo watu wanabanana kwenye mabasi kutokana na kutokuwapo usafiri mwingine rahisi na wa haraka katika njia hii baada ya kuondolewa kwa daladala.”

Kicheko Mbagala

Katika hatua nyingine, mradi wa Dart njia ya Mbagala, Karugendo alisema umeshakamilika kwa asilimia 78 na vitu vilivyobaki ni vidogo, vikiwamo vivuko vya Uhasibu, Mbagala Rangi Tatu na Kigogo.

Baada ya kuanza kazi kwa barabara hiyo, alisema mabasi 750 yanatarajiwa kuingia barabarani kusafirisha abiria 600,000 hadi 700,000 kwa siku.

“Idadi hiyo ya mabasi itakuwa ikihudumia barabara zote, zikiwamo zile za mlisho za kuwafikisha abiria vituo vikuu na baadaye kama kutakuwa na uhitaji zaidi tutaongeza,” alisema Karugendo.

Chanzo: mwanachidigital