Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa kufanya mageuzi makubwa katika mazao ya mafuta ikiwemo michikichi na kuzalisha mafuta ya kutosha.
Akiwa Mkoani Kigoma, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wenye ardhi inayokubali zao hilo wafanye hivyo mara moja kwani mbali na kuwapa fedha za uhakika, litaleta fursa ya ajira kupitia viwanda vinavyofunguliwa “Chikichi ni fursa, chikichi ni maendeleo, ni fursa ya kuleta viwanda hapa Kigoma na kwenye mikoa mingine itakayolima zao hili, chikichi ni uchumi, ni uchumi wa Mtu mmojammoja na uchumi wa kitaifa”
Serikali ilichukua hatua za makusudi za kuliingiza zao la michikichi katika orodha ya mazao ya kimkakati, mazao mengine ya kimkakati ni pamba, tumbaku, kahawa, korosho, chai, mkonge, zabibu na alizeti.
Akizungumzia kuhusu mahitaji ya mafuta ya kula nchini, Waziri Mkuu amesema “Hivi sasa mahitaji ya mafuta nchini ni zaidi ya tani 650,000 huku uzalishaji ukikadiriwa kuwa tani 290,000 tu, hivyo, kiasi cha tani 360,000 sawa na 55.4% huagizwa kutoka nje ya nchi na kuigharimu Serikali takribani shilingi bilioni 470 kila mwaka, tunahitaji hii fedha iendelee kutumika nchini”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na Wadau, Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde alisema Wizara hiyo inaendelea na uzalishaji wa mbegu na miche bora ya michikichi aina ya TENERA inayotoa mafuta mara tatu zaidi ya aina ya DURA ambayo inalimwa na Wakulima kwa takribani asilimia 90.