Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanza yasafirisha tena tani 20 minofu ya samaki kwenda Ubelgiji

RWAN.webp Mwanza yasafirisha tena tani 20 minofu ya samaki kwenda Ubelgiji

Tue, 19 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ndege ya Rwanda A330-300 yenye usajiri 9xR-WP imerejea tena nchini na kuondoka na tani 20 za minofu ya samaki ambapo gharama ya mzigo na usafirishaji kwenda Brusels nchini Ubelgiji umegharimu kiasi cha USD 80,200.

Mzigo huo ni kutoka katika kampuni ya Tanzania Fish Processors Ltd ambayo imesafirisha tani 16 na Nile Perch Fisheries Ltd tani 4.

Akizungumza baada ya kushuhudia ubebwaji wa mzigo huo kwa awamu ya pili Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi jengo la mizigo katika uwanja wa ndege wa Mwanza ambapo ndege yoyote duniani inaweza kutua katika eneo hilo.

Amesema tija ndio inaanza kuonekana kwa rasilimali kutumika ipasavyo,sambamba na wenye viwanda vya samaki kuanza kuona thamani ya kusafirisha bidhaa zao kutumia uwanja huo baada ya mara kadhaa mizigo yao kukosa ndege pindi walipokuwa wakifuata huduma kama hiyo nchi jirani kama Kenya.

"Haya ni maono ya Rais na ni maelekezo yake ya muda mfupi ambayo utekelezaji wake umefanyika kwa uharaka pia biashara imeanza kufufuka huku wadau wakipenda uwanja huku mahitaji nayo yanazidi kuwa makubwa hivyo wakazi wa Mwanza wachangamkie fursa hii kikamilifu,"amesema Mongella.

Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli nchini ( MSCL) Eric Hamissi, amesema Tanzania ni nchi tajiri na imeweza kufanya mambo makubwa kwa kusafirisha minofu ya samaki lakini baadae watasafirisha nyama ya ng'ombe na mbuzi hayo ni mapindizi yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano.

Naye Meneja wa Nile Perch Fisheries Ltd, Ruesh Mohan amesema usafirishaji wa mizigo kutoka Mwanza inawapunguzia gharama za usafirishaji na pia ameitaka Serikali kuangalia namna ya upatakanaji wa usafiri kwa wiki mara mbili.

Ameongeza kuwa mbali na soko kushuka baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu COVID -19 bado sekta ya uvuvi inauwezo wa kusafirisha tani 100 hadi 150 kwa wiki kutoka Mwanza kwenda Ulaya .

Kwa upande wake Meneja Rasilimali watu kutoka Tanzania Fish Processors Ltd, Godfrey Samwel amewataka wavuvi kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali kwa kuwa usafiri wa uhakika wa kutoa samaki kwenda ulaya upo.

Amesema uzalishaji utakapokuwa mkubwa utaongeza usafirishaji wa bidhaa hiyo kwa sababu tutakuwa na malighafi za kutosha sambamba na hilo ameiomba serikali kuangalia namna ya kuwa na ndege ya ndani itakayosafirisha mzigo kwenda nchi mbalimbali za ulaya ili kuweza kukuza uchumi wa nchi.

"Tulianza na tani 8 leo tunasafirisha tani 16 ambapo mzigo pamoja na usafirishaji gharama zake ni USD 64200, hivyo imani yao ni kuendelea kusafirisha mzigo mkubwa zaidi mwanzo tulipata taabu sana tulisafirisha mzigo kwa njia ya malori kwenda Nairobi wakati mwingine gari linaharibika njiani, mzigo kuharibika na kutofika kwa muda,"amesema Samwel.

Meneja wa Uwanja wa Ndege Mwanza, Pascal Kalumbeta amesema Serikali kwa ushirikiana Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania imeweka miundombinu ya kisasa inayowezesha ndege aina yoyote na yenye ukubwa wowote kuweza kutua katika kiwanja hicho.

Ameongeza kuwa jengo hilo lina uwezo wa kuhifadhi mizigo inayoharibika kwa haraka pamoja na mizigo inayokaa kwa muda mrefu hivyo alizitaka sekta binafsi ,wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo na kutengeneza soko la kimataifa.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Murilo Jumanne Murilo amesema kulingana na shughuli kubwa za kiuchumi wamejiimalisha zaidi katika masuala ya ulinzi na shughuli hizo hazitapata matatizo ya kiusalama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live