Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanadiplomasia wa uchumi aipa mbinu ya masoko Tantrade 

A55a22b2402799075e8d8c1f2425a7b7.jpeg Mwanadiplomasia wa uchumi aipa mbinu ya masoko Tantrade 

Fri, 30 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKURUGENZI wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi, Balozi Edwin Rutageruka ametoa wito kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) kuimarisha Kitengo cha Intelijensia ya Masoko cha mamlaka hiyo ili kishirikiane na waambata wa biashara kwenye Balozi za Tanzania kwenye nchi mbalimbali.

Balozi Rutageruka ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, alitoa ushauri huo juzi wakati akikabidhi ofisi kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Latifa Khamis.

Alisema ndoto yake ilikuwa kuifanya TanTrade kuwa na chanzo cha mapato zaidi ya kimoja na kumshauri Latifa kusimamia ukamilishwaji wa miradi ya maendeleo kikiwamo Kituo cha Nafaka cha Gairo mkoani Morogoro, Kilimanjaro Business Park mkoani Kilimanjaro na Kurasini Export House, Dar es Salaam.

Miradi mingine aliyoitaja ni Kituo cha Biashara cha Wajasiriamali, mradi wa kuendeleza Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Nyerere (SabaSaba), pamoja na kusimamia ujenzi wa mradi wa Uwanja wa Maonesho ya Kimataifa uliopo Fumba, Zanzibar.

Pia aliitaka Tantrade kusimamia miradi ya uwezeshaji biashara nchini ukiwamo wa Tanzania Trade Information Portal, Tanzania Spice Label na wa E-Shop wa Shirika la Posta.

Kwa upande wake, Latifa aliwataka wafanyakazi wa TanTrade kufanya kazi kwa uadilifu na ushirikiano ili kuiwezesha mamlaka hiyo kujenga mazingira wezeshi ya biashara nchini.

Alisema kufanya kazi kwa bidii kutawezesha kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa wakati na kuwaonya wenye tabia ya uvivu na uzembe.

Chanzo: www.habarileo.co.tz