Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwambe azungumzia sera ya viwanda vidogo

B5283cdaf0e13133f6f7a1c361cd4beb Mwambe azungumzia sera ya viwanda vidogo

Sat, 19 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Goffrey Mwambe ametaka Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo kuwa mkombozi wa kipato cha mtu mmoja na kusaidia nchi kufika uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2025.

Mwambe aliyasema hayo wakati wa kufungua mkutano wa wadau wa kujadili rasimu ya Sera ya Maendeleo ya viwanda vidogo na biashara ndogo, ambayo inalenga kushughulikia mapungufu ya sera ya wajasiriamali ya mwaka 2003 iliyojengwa kwenye eneo moja la sekta ya uzalishaji viwandani.

“Sera ya Ujasiriamali ya mwaka 2003 ilikuwa imejengwa kwenye eneo moja la sekta ya uzalishaji viwandani, wakati ujasiriamali uko katika nyanja mbalimbali ikiwamo kilimo, ufugaji na kwenye utoaji huduma. Hivyo tunataka sera inayoandaliwa iwe mkombozi kwa kipato cha mtu mmoja mmoja na kusaidia nchi kufikia uchumi wa juu na kuondoa umasikini na kuboresha ustawi wa Watanzania,” alisema.

Mwambe alisema sera hiyo pia inatakiwa kuwatambua, kuwasajili na kuwatengeneza mazingira wezeshi wajasiriamali katika kufanya shughuli zao.

“Tunataka sera iwatambue na kuwasajili na tuimarishe na MKURABITA, mkakati wa kutambua na kuratibu wajasiriamali,” alisema na kuongeza kuwa sera inapaswa kutambua na kurasimisha biashara na shughuli za wajasiriamali

“Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zina idadi kubwa ya wananchi wake ambao wako katika sekta isiyo rasmi na tukiwatengenezea mazingira hawa tutawafanya kuongeza kipato na nawawazia kufikia kipato cha Dola za Marekani 2,995 hivyo nchi kufikia uchumi wa kati wa juu. Tunataka sera hii iweze kuwajenga wajasiriamali kwenye mfumo wa kukua na kuwe na mpango wa thabiti kuhakikisha wanakua, kupata urahisi wa huduma za kifedha, kupata taarifa za masoko na kuunganishwa na masoko,”alisema.

Alisema pia sera hiyo inatakiwa kuwajenga wawekezaji wa ndani wajao na kufanya hivyo, kutaongeza wigo wa biashara na wigo wa walipa kodi.

Mwambe alisema sera hiyo inapaswa kuwaunganisha wadau na taasisi zote zinazoshughulika na usimamizi na udhibiti na kubainisha majukumu ya kila mdau, ambayo yatawekewa utaratibu wa kuitathimini utekelezaji wake.

Katibu Mkuu, Profesa Riziki Shemdoe alisema hatua ya kuandaa sera hiyo ni kuzidi kuinua sekta ya ujasiriamali ili iweze kuchangia zaidi pato la taifa.

Chanzo: habarileo.co.tz