Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwaka 2019 ulivyotingisha sekta ya korosho Tanzania

90142 Korosho+pic Mwaka 2019 ulivyotingisha sekta ya korosho Tanzania

Sat, 28 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Sekta ya korosho nchini inaendelea kuuguza madhara ya matukio ya msimu wa 2018/19 wakati Serikali iliponunua tani 222,000 kati ya tani 225,000 za korosho zilizozalishwa nchini.

Hatua hiyo ilichukuliwa na Serikali ili kulinda maslahi ya wakulima baada ya wanunuzi kutoa bei ndogo katika minada ya awali, hali iliyotafsiriwa kuwa ni mpango wa kutaka kuwanyonya wakulima.

Uamuzi wa kununua korosho hizo ulitangazwa Novemba 2, 2018 na Rais John Magufuli na kuiagiza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali kununua korosho zote kwa bei ya Sh3,300 kwa kilo.

Katika mchakato huo, TADB ilishirikiana na Wizara ya Kilimo, wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Mipango na Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Pia ilishirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CBT), Bodi ya Leseni za Maghala Tanzania (WRRB) na Kampuni ya Soko la Bidhaa Ghafi (TMX).

Hata hivyo, wakati mwaka huu ukielekea ukingoni, Tanzania imeendelea kushughulikia changamoto zilizotokana na matukio ya msimu uliopita.

Changamoto hizo ni pamoja na kushuka kwa uzalishaji katika baadhi ya maeneo kama wilaya ya Tandahimba na Newala zinazokuwa kinara wa uzalishaji.

Changamoto nyingine ni pamoja na kushindwa kufikiwa kwa bei ya Sh3,300 iliyolipwa na Serikali msimu uliopita, ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima na upungufu wa vifungashio.

Pia, tumeshuhudia mfumo wa mauzo ya korosho ghafi mtandaoni ukisitishwa, kufutwa kazi kwa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda na kusitishwa kwa utaratibu wa kuwasilisha zabuni kwenye ofisi za wakuu wa mikoa (RCs) na Wakuu wa Wilaya (DCs).

Uzalishaji mdogo wa korosho

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred aliliambia Mwananchi mwanzoni mwa mwezi Desemba kuwa tani 151,574.164 zenye thamani ya zaidi ya Sh406.330 bilioni ziliuzwa kwa mnada kufikia Desemba 8, 2019.

Alielezea wasiwasi kuwa inawezekana wakashindwa kufikia lengo walilojiwekea la kuzalisha tani 290,000 msimu huu, hasa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyosababisha karibu tani 5,000 kuharibika mkoani Pwani.

Takwimu zilizotolewa na viongozi wa vyama vya ushirika zinaonyesha kuwa Chama cha Ushirika cha Masasi na Mtwara (Mamcu) kimeuza zaidi ya tani 68,000 hadi kufikia mnada wa nane na wenzao wa Tandahimba na Newala waliuza tani 51,914 kati ya tani 80,000 walizotarajia kukusanya msimu huu.

Nacho Chama cha Ushirika Tunduru (Tamcu) kimeuza tani 17,000 kati ya tani 23,000 zilizotarajiwa huku Chama cha Ushirika cha Ruangwa, Nachingwea na Liwale (Runali) kikiuza tani 25,000 kati ya tani 45,000 zilizokadiriwa.

Viongozi wa vyama vya ushirika wamesema ni vigumu nchi kufikia malengo ya kuzalisha karibu tani 300,000 lililowekwa kwa msimu wa 2019/20.

Wakulima wamehusisha kushuka kwa uzalishaji katika baadhi ya maeneo na ucheleweshaji wa malipo ya msimu wa 2018/19 kulikosababisha wachelewe kufanya maandalizi ya mashamba yao kwa ajili ya msimu wa 2019/20 ikiwa ni pamoja na ununuzi wa pembejeo.

“Hata pale ukopeshaji wa pembejeo ulipotangazwa na CBT, bado kulikuwa na urasimu mkubwa kupata pembejeo hizo, hali iliyofanya wakulima wengi kushindwa kupulizia mashamba yao dawa kama inavyotakiwa na kwa wakati,” alisema Ally Kaisi kutoka Chama cha Msingi cha Mitondi ‘A’ (Amcos).

Kushuka kwa uzalishaji si tu kumewanyima mapato ya kutosha wakulima hao, bali kutapunguza mapato ya Serikali yatokanayo na usafirishaji korosho nje ya nchi (export levy).

Msimu wa 2017/18, Serikali ilipata dola 575 milioni za Kimarekani kwa kusafirisha korosho nje ya nchi (sawa na Sh1.3 trilioni).

Msimu wa 2018/19 Serikali ilitumia Sh722 bilioni kununua korosho ghafi kutoka kwa wakulima kwa bei ya Sh3,300 kwa kilo.

Korosho zauzwa bei ya chini

Hadi kufikia mnada uliofanyika Desemba 8, tasnia ya korosho haijaweza kufikia bei ya Sh3,300 iliyotolewa na Serikali msimu uliopita.

Bei ya chini msimu huu ni Sh2,047 iliyopatikana kwa Chama cha Ushirika Pwani (Corecu), huku bei ya juu ya Sh2,857 ikifikiwa na Chama cha Ushirika Runali katika mnada wake wa Desemba 1, 2019.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa bei imekuwa tofauti kwa Sh1,253 na Sh443 ikilinganishwa na bei ya Sh3,300 ya msimu uliopita.

Msimu mpya ulioanza Oktoba 31, 2019 ulishuhudia ucheleweshwaji wa malipo, huku baadhi ya wakulima wakilalamikia kutolipwa kwa fedha za korosho zilizouzwa minada miwili hadi mitatu nyuma tofauti na ahadi ya Serikali kulipa siku kumi baada ya mnada.

Mrajisi msaidizi wa ushirika mkoani Mtwara, Juma Mokili alisema kikao cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mabenki yanayohusika na mauzo ya korosho kimeshatatua changamoto hiyo.

“Tatizo ni kwamba benki nyingi hazina matawi maeneo mengi ya vijijini na kuna baadhi ya wakulima hawakutoa taarifa sahihi ya akaunti zao. Hata hivyo, suala hilo limefanyiwa kazi na sasa malipo yanaharakishwa,” alisema.

Awali, kaimu mkurugenzi wa CBT, Alfred alisema wametoa namba maalumu itakayowawezesha wakulima kuripoti ucheleweshaji zaidi wa malipo yao ili yashughulikiwe mara moja.

Sekta ya korosho ilikabiliwa na upungufu mkubwa wa magunia, hivyo kuibua hofu kuwa korosho zinaweza kuharibika majumbani ama wakati wa usafirishaji.

Tatizo hilo lilionekana kuwa kubwa zaidi wilayani Tunduru ambako viongozi wa ushirika waliambatana na Mkuu wa Wilaya Julius Mtatiro kuja Dar es Salaam kufuatilia vifungashio hivyo.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi walihusisha upungufu huo na deni la karibu Sh7.9 bilioni lililotokana na magunia yaliyotumika msimu wa 2017/18 na 2018/19.

Itaendelea...

Hata hivyo, waziri wa Kilimo Japhet Hasunga alipinga vikali madai hayo na kusema deni hilo halina uhusiano na upungufu uliojitokeza.

“Vyama vya ushirika vinapaswa kukiri uzembe waliofanya ikiwa ni pamoja na kutoishirkisha serikali kwa wakati. Hata hivyo, mzabuni amehakikishiwa malipo na tatizo linaekea kumalizika,” alisema mara baada ya kuwasili mkoani Mtwara.

Aliongeza, “Natarajia pia kukutana na viongozi wa vyama vya ushirka ili kujadiliana na kuafikiana nao kuhusu madeni ya vifungashio ya misimu iliyopita.”

Mauzo ya korosho kwa njia ya mtandao yaahirihswa

Akitangaza kuanza kwa msimu mpya wa korosho jijini Dar es Salaam, Septemba 20, 2019, waziri Hasunga alisema korosho zitauzwa kwa njia ya mtandao kupitia Kampuni ya soko la Bidhaa Ghafi nchini (TMX).

Alifafanua kuwa mfumo huo unalenga kuongeza uwazi na kuwapa fursa wakulima kuchagua mteja aliyeweka bei ya juu kuliko wote.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kusitishwa kwa mfumo huo alipowahutubia wananchi mjini Mtwara Oktoba 2, 2019 ili kutoa nafasi kwa wakulima na wanunuzi kuelimishwa zaidi kuhusu mfumo huo.

Hatua hiyo ya Waziri Mkuu ilikuja kufuatia malalamiko ya wakulima kwamba wadau hawakuelimishwa vya kutosha kuhusu mfumo huo hivyo kuwepo uwezekano wa kudhulumiwa.

Waziri Kakunda afutwa kazi

Juni 8, 2019, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda kwa kile kilichokuja kubainika kuwa ni kushindwa kusimamia mauzo ya korosho zilizonunuliwa na serikali.

Nafasi yake ilichukuliwa na aliyekuwa naibu waziri wa Kilimo Innocent Bashungwa ambaye pamoja na Kamishina Mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Edwin Mhede waliapishwa Juni 10, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema, “Tumenunua zaidi ya tani 200,000 za korosho, lakini ni kiasi gani kimeuzwa? Akiwa waziri wa Viwanda na Biashara (Kakunda) amefanya biashara gani ya korosho?” alihoji na kuendelea.

“Wizara ya Kilimo na Jeshi la wananchi wa Tanzania wametimiza majukumu yao ya kukusanya korosho na kuzihifadhi kwenye maghala. Lakini nini kimefanywa na wizara ya Viwanda na Biashara?”

Alisema bidhaa hiyo imerundikana kwenye maghala hadi Machi mwaka huu ambapo masoko ya zao hilo kwenye nchi za Benin, Nigeria na Ivory Coast yamefunguliwa.

“Kuna maana gani ya kuwa na wizara hii” Nadhani Innocent (Bashungwa) anastahili kuhurumiwa badala ya kupongezwa,” alisema Rais Magufuli.

Magufuli azikatalia wizara, bodi ya korosho

Akiwa katika ziara mkoani Lindi, Rais Magufuli aliiagiza wizara ya Kilimo na CBT waachane na mpango wa kuweka masanduku ya tenda kwenye ofisi za wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya zinazolima zao hilo.

Aliwataka viongozi wa taasisi hizo kuweka utaratibu mwingine na kubainisha kuwa licha ya kuchochea rushwa, utaratibu huo unatoa nafasi kwa watu wachache kufanya maamuzi kuhusu zao hilo.

Marekebisho yalifanyika ambapo masanduku sasa yalielekezwa yawekwe kwenye eneo la mnada ambapo chama cha ushirika husika kitakuwa na jukumu la kuanzisha mchakato saa 2 asubuhi na kuufunga saa 10 jioni.

Wadau wafunguka

Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima Tandahimba (Taffa) Faraji Njapuka alisema 2019 ulikuwa mwaka mgumu kwa wakulima wa zao hilo kutokana na ucheleweshaji wa fedha za korosho zilizouzwa msimu wa 2018/19 kulikosababisha maandalizi ya mashamba kuchelewa.

“Wakulima wengi walishindwa kununua pembejeo kwa wakati hali iliyochangia mavuno kupungua msimu wa 2019/20 hasa katika wilaya za Tandahimba na Newala,” alisema.

Aliongeza, “Hata msimu mpya ulipoanza malipo yalichelewa vilevile tofauti na maelekezo ya serikali kwamba yafanyike siku 10 baada yam nada kufanyika.”

Meneja mkuu wa Mamcu Protence Rwiza alisema chama chake kimepata neema kubwa msimu huu baada ya kuuza zaidi ya tani 68,000 kufikia mnada wa nane.

“Ni rekodi ambayo haijafikiwa na vyama vyote vya ushirika msimu huu. Zaidi ya changamoto ya magunia ambayo tuliimaliza, hatuna tatizo lingine kwa sababu malipo ya wakulima yanakwenda vizuri,” alisema.

Meneja mkuu wa Runali, Hassan Mpako alisema mfumo wa stakabadhi ghalani uliotumika msimu huu umeboreshwa na kuongeza uwazi na kuondoa dhana ya wanunuzi kupanga bei.

“Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo ni kasi ndogo ya wanunuzi kusomba korosho kwenda kwenye maghala ya vyama vya ushirika. Matokeo yake mvua zimeanza kunyesha hali inayotishia kuharibu ubora wa korosho zinazoendelea kusombwa,” alisema.

Naye meneja mkuu wa Tamcu, Imani Kalembo alisema baada ya kutatua changamoto ya magunia, ana uhakika wa kuvuka lengo walilojiwekea la kuuza tani 23,000 msimu huu ikilinganishwa na tani 18,000 msimu uliopita.

Mwenyekiti wa Tanecu, Shaibu Aifai alisema ucheleweshaji wa malipo umeleta changamoto kubwa ya kijamii na kiuchumi miongoni mwa wanachama wake.

“Serikali inapaswa kuviamini vyama vya ushirika kuwa vina uwezo kulisimamia zao la korosho. Pia inapaswa kupunguza matamko ambayo yameshamiri kwenye korosho kuliko zao lingine lolote nchini hali inayowachanganya wadau,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz