Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvutano wa umiliki Soko la Sinza 1

Soko Balaaa.jpeg Mvutano wa umiliki Soko la Sinza 1

Tue, 21 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mvutano wa umiliki umezuka kati ya Manispaa ya Ubungo na wananchi wanaodai kumiliki fremu za biashara katika soko la Sinza 1 jijini Dar es Salaam.

Mvutano huo umetokana na kile kinachoelezwa na wananchi hao kuwa manispaa hiyo imekwenda ghafla kusainisha mikataba inayowatambua wamiliki wa maeneo hayo kama wapangaji.

Akizungumza nasi sokoni hapo, Mwenyekiti wa Wamiliki hao, Yusuph Nyalori alisema kinachowashangaza ni mikataba inayosainishwa kuondoa umiliki wao na kuuhamishia kwa manispaa.

“Sisi tumejenga kwenye maeneo haya tangu kabla ya miaka ya 1970, hata soko hili halikuwepo, eneo hili lilikuwa la wazi tu wakati huo kama ushoroba (uchochoro),” alisema.

Alisema nwaka 1975 hadi 1977 wakati maeneo yanapimwa, eneo hilo kulipatikana huduma mbalimbali kutokana na kuwepo maduka na magenge.

Nyalori alisema baadaye eneo hilo likiwa chini ya halmashauri ya Kinondoni, likatakiwa kuwa soko na wamiliki hao walitozwa Sh50 kila siku kama ushuru kwa kila kibanda.

“Baadaye Kinondoni ilikuja kutaka kurasimisha eneo hilo ili liwe soko na kila mfanyabiashara alitozwa Sh200 kama atakuwepo sokoni kufanya shughuli zake.

Kwa makubaliano hayo, alisema mahakama iliwatambua wananchi hao kama wajenzi na kwa kuwa eneo la soko kila kibanda barabarani kilitozwa Sh50,000 na vilivyopo ndani Sh25,000.

Katika hali isiyoeleweka, alisema juzi maofisa kutoka manispaa walifika sokoni hapo na mikataba wakawakamata baadhi ya wafanyabiashra kwa madai ya kudaiwa kodi na kisha kuwapa mikataba yenye nyongeza ya kodi kutoka Sh50,000 hadi 75,000 na Sh25,000 hadi Sh50,000.

“Tulikaa vikao mara kadhaa na manispaa na tulikubaliana bei zile zilizokuwepo awali, hizi bei mpya hatukuwahi kukubaliana, tunashangaa wamekuja nazo, lakini mbaya zaidi anayesainishwa mkataba ni yule atakayekutwa eneo la biashara si mmiliki wa eneo,” alisema.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mansipaa ya Ubungo, Beatrace Dominick alisema hakuwa kwenye eneo zuri la kuzungumza.

“Nipo kwenye kelele siwezi kuongea,” alijibu na hata alipotafutwa baadaye simu yake iliita bila majibu.

Hata hivyo, Mwananchi lilizungumza na mmoja wa maofisa wa manispaa waliokuwepo kwenye operesheni hiyo, akisema kinachofanywa ni utekelezaji wa makubaliano kati ya pande mbili.

“Maeneo yote ya masoko yanamilikiwa na manispaa na kuna sheria ndogondogo nyingi zinazofafanua hiki kinachofanyika na hizi sheria zilitungwa kwa kuzingatia maoni ya hawahawa, wanachokifanya hapa ni ubishi tu,” alieleza ofisa huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live