Dar es Salaam. Usafiri wa treni kati ya Dar es Salaam na Morogoro utakosekana kwa takriban wiki mbili baada ya reli kuharibiwa tena na mvua zinazoendelea kunyesha kote nchini.
Hii itakuwa ni mara ya pili katika miezi michache baada ya Shirika la reli (TRC) kulazimika kurudishia wasafiri nauli ili wawe kumalizia safari zao za kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kati kwenda Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka jana.
TRC imesema kuwa maeneo 26 korofi yaliyo katika eneo la kilomita 120 yameharibika vibaya na yanahitaji matengenezo ili usafiri uweze kurudi katika hali ya kawaida.
Reli ya kati huhudumia abiria na mizigo katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mwanza na Kigoma.
Mkurugenzi mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema jana kuwa tayari wameanza kuhamisha reli katika baadhi ya maeneo yaliyoharibiwa na ujenzi huo utakamilika ndani ya siku 7 hadi 10 kama mvua hazitaendelea kunyesha.
“Reli yote iliyoharibiwa-- kilomita 120-- itahamishwa kuwekwa mlimani, iwe kama reli ya standard gauge (SGR),” alisema Kadogosa.
Pia Soma
- Majaliwa awataka wanaoishi mabondeni kuhama
- Wanaume waaswa kupima saratani ya matiti
- Rais TLS ataka sheria, haki kuheshimiwa
Tuta linalopita karibu na Mto Mkondoa mkoani Morogoro limesombwa na maji na kuharibu reli hiyo katika maeneo ya Kilosa, Gulwe, Igandu, Zuzu na Matukupora.
Kuhusu abiria waliokwama, alisema baadhi walitafutiwa mabasi kumalizia safari zao na ambao walikuwa wasafiri juzi wamerudishiwa nauli zao.
Hata hivyo, Kadogosa alisema treni za Dar - Kilimanjaro, Dar - Tanga na Mpanda - Tabora - Mwanza zinaendelea kutoa huduma kama kawaida kusafirisha mizigo na abiria. Alisema reli katika maeneo hayo iko salama.
“Tunaangalia uwezekano wa kuendelea na huduma kuanzia Dodoma kwenda maeneo mengine kama Kigoma na Mwanza,” alisema Kadogosa, akiwatoa wasiwasi abiria na wafanyabiashara katika maeneo hayo.