Watoto 37 wamekufa katika kipindi cha Januari hadi Aprili, mwaka huu kwa kusombwa na maji, kutumbukia kwenye visima au mashimo yaliyojaa maji katika maeneo tofauti nchini kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Dodoma na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime, imesema matukio hayo yameripotiwa kutokea katika mikoa tisa nchini ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Kigoma, Mwanza, Pwani, Katavi, Morogoro na Rukwa.
Akizungumzia matukio hayo, Kamanda Misime alisema uchunguzi umebaini kuwa mashimo yaliyochimbwa hayafukiwi wala kuwekewa tahadhari au uzio ili kuepusha madhara.
“Kibaya zaidi watoto hawapewi uangalizi kutoka kwa baadhi ya wazazi au walezi na matokeo yake hujikuta wamepata madhara yakiwepo hayo ya kupoteza maisha kwa kutumbukia kwenye mashimo, madimbwi au kusombwa na maji,” alisema Misime.
Alisema katika kipindi hiki cha msimu wa mvua na katika misimu mingine wazazi na walezi wahakikishe wanatimiza wajibu wao wa kuwalinda watoto kwa sababu ni takwa la kisheria na kidini na kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kushindwa kulitekeleza na kusababisha watoto kupata madhara.
Aidha, jeshi hilo linatoa tahadhari na onyo kwa wananchi wachache wanaoendelea kutumia vibaya mitandao ya kijamii na kusababisha hofu, taharuki na mahangaiko yasiyo ya msingi kwa wengine.
“Mfano tumeshuhudia hivi karibuni baadhi ya watu wanatafuta picha za matukio ya zamani tena yaliyotokea katika nchi nyingine na kurusha kwenye mitandao ya kijamii na kuandika ni tukio la hivi punde limetokea mkoa fulani,” alisema Misime.
Alisema katika mifano hiyo kuna taarifa imerushwa hivi karibuni ikionesha gari aina ya Toyota Landcruiser Hard top likisombwa na maji, mhalifu aliyetengeneza uongo huo aliandika tukio hilo limetokea muda mfupi huko Arusha wakati ukweli ni kwamba tukio hilo lilitokea mwaka jana Afrika Kusini.
“Mhalifu huyu amewaletea hofu watu kitendo ambacho si cha kiungwana katika jamii iliyostaarabika, watumiaji vibaya wa mitandao ya kijamii kama hawa inabidi jamii iendelee kuwakumbusha kuwa kuna baadhi ya binadamu wenzao wana magonjwa na wanapopata taarifa za kushtua kama hizo wanaweza kupata madhara makubwa na kupoteza maisha,’’ alisema Kamanda Misime.
Hivyo akawataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za wahusika wanaosambaza matukio ya uongo katika mitandao ya kijamii ili wahusika wachukue hatua stahiki na kusema Jeshi la Polisi linawataka wenye tabia hiyo ya kuzusha uongo kuacha mara moja.