Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yapaisha bei ya sukari Kilimanjaro

Sukarii Sukari Leseni Mvua yapaisha bei ya sukari Kilimanjaro

Thu, 14 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mvua zinazoendelea kunyesha nchini, zimesababisha kuadimika kwa sukari mkoani Kilimanjaro huku bei ikipanda hadi Sh4,000 kwa kilo moja katika baadhi ya maeneo kutoka Sh2,800 na Sh3,000.

Awali, Kiwanda cha sukari Moshi (TPC) kililazimika kusimamisha uzalishaji kwa siku 30 baada ya mashamba kujaa maji ya mvua na kusababisha miwa kuoza. Hata hivyo, Ofisa Mtendaji anayeshughulikia Utawala TPC, Jaffary Ally alisema,

“tumeanza uzalishaji na Jumatatu tunaanza mauzo. Kwa wale waliochukua advantage (manufaa) ya kiwanda kusimama na wao kupandisha bei, waache biashara hiyo mara moja.”

Wakati walaji wa Kilimanjaro wakilalamika kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo, mikoa mingine ukiwamo wa Dar es Salaam kilo moja ya sukari kwa bei ya rejareja inauzwa kati ya Sh2,800 hadi 3,000.

Mbali ya kupanda bei ya reja reja Kilimanjaro, ya jumla kwa mfuko wa kilo 25 nayo imepanda kutoka Sh60,000 hadi Sh83,000.

Kutokana na bei ya jumla kupanda, wauzaji wa reja reja wamelazimika kupandisha bei kati ya Sh3,500 na Sh4,000 kwa kilo huku sukari iliyoko sokoni kwa sasa ni ya Kilombero na Bagamoyo.

Mfanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina la baba Majani, alisema kwa sasa sukari imepanda bei kwa kile walichoelezwa na wauzaji wa jumla kuwa TPC wamefunga kiwanda.

"Sukari hapa nauza kilo moja kwa Sh3,500 ya kupima na ile ya pakiti nauza Sh3,700... na kushuka bei ni mpaka wauzaji wa jumla nao wapunguze bei,"alisema mfanyabiashara huyo.

Juliana Massawe anayemiliki duka la rejareja, alisema jana alinunua mfuko wa kilo 25 kwa Sh82,000 na kilo 50 kwa Sh157,000 hivyo analazimika kuuza kilo moja kwa Sh4,000.

Mmoja wa wauzaji wakubwa Kilimanjaro aliyekataa jina lake lisitajwe alisema kwa sasa inawalazimu kuagiza sukari Bagamoyo katika Kiwanda cha Azam kutokana na sukari ya TPC kuadimika.

“Kwa sasa sukari imeadimika, hii ni kutokana na TPC kupata hitilafu na kushindwa kuzalisha kwa muda sasa, na hiyo imefanya sukari ipande bei kwa sababu ya gharama za usafirishaji,"alisema.

Kauli ya RC Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya sukari na kutoa onyo kwa wafanyabiashara. Babu aliwataka wafanyabiashara hao kuacha kuwalangua wananchi kwa bei ya juu ya sukari akisema Serikali haijatangaza kupanda kwa bei elekezi ya bidhaa hiyo.

"Nimepata taarifa kutoka kwenye Kiwanda cha Sukari TPC, kuwa kutokana na wingi wa mvua, miwa yote ilikuwa imeoza, hivyo haiwezi kuzalisha sukari, kwa hiyo kiwanda kikafungwa,”alisema Babu.

“Akiba waliyokuwa nayo yote waliitoa wakabakiwa na akiba kidogo ya dharura. Lakini kuanzia juzi (Jumatatu) kiwanda kimeanza kufanya kazi, na uzalishaji umeanza,” alisema Babu.

Pia, alisema baada ya siku mbili au tatu kuanzia jana, sukari itakuwa inasambazwa ya kutosha.

"Nimepata malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa sukari imepanda na ukienda kununua sukari unaambiwa ununue na sindano sijui kiwembe (kupewa sharti la kununua bidhaa nyingine ili uuziwe sukari kutokana na kuadimika) vitu ambavyo havihusiani na sukari,” alisema Babu.

“Serikali haijatangaza kupandishwa kwa bei ya sukari, bei ya sukari ni ile ile na mwananchi ainunue kwa bei ya kawaida na hakuna kumuongezea kitu kingine cha kununua," alisisitiza.

TPC wafunguka kila kitu

Akizungumza n jana baada ya kutakiwa kueleza nini kimesababisha sukari kuadimika, Ally ambaye ni Ofisa Mtendaji wa TPC, alitaja kiini ni mvua kubwa zinazonyesha.

“Ni kwamba mvua hizi za vuli ambazo sasa hivi wanasema ni za El-Nino na sisi tumepata excessive rain (mvua nyingi) huku kwetu.

“Tumepata mvua nyingi kuliko miaka karibia yote kwa kipindi cha Oktoba na Novemba. Kwa hiyo tulisimama uzalishaji, muda wote mvua zinanyesha na katika mashamba huwezi kuingiza matrekta; na kuna miwa ililala wiki tatu shambani. Imeharibika. Kwa hiyo mashamba matatu yalikuwa yamelaza miwa tani 7,000,” alieleza Ally.

“Kwa hiyo huo mua tunaubeba hivyo hivyo ukiwa umeharibika kuuleta kiwandani ili kui-crash (kuivunja vunjana kukamua) kupata molasses na pumba za kuzalishia umeme.”

“Sasa katika ile ku-crash mashine yetu na yenyewe ikafanya vibration (kutetemeka) ikabidi kusimama. Kuifungua wakasema inabidi mbadilishe rotter tukabadilisha. “Tulipowasha tukakuta bado inatetemeka. Wataalamu wakasema inabidi itafutwe mashine kutoka Israel tulipowasiliana nao bahati nzuri wakasema iko hapo Kenya,”alieleza Ally.

“Tumewaomba sasa watuletee inakuja. Wakati tunasubiria mashine ikabidi tufungue kiwanda tuanze kuzalisha kwa kutumia umeme wa Tanesco bahati mbaya nao wako kwenye mgawo.

“Wakatuambia TPC mnahitaji megawati 12 kwa hiyo wakizitoa hizo kutupa ina maana wataingia kwenye upungufu wa megawati 30,” alisema Ally.

“Kwa maana hiyo wakatuambia kama wakitupa hizo megawati 12 maana yake mkoa mzima wa Kilimanjaro utakuwa gizani. Kwa hiyo ikabidi tusubiri wajadiliane na makao makuu.”

Ally alisema walisubiri na Desemba 11 ndio wakapewa megawati nane badala ya 12 na huo upungufu unawalazimu kutumia jenereta za kiwanda na ndio wameanza uzalishaji.

“Katika stock (akiba) ndio ajabu ilipo. Miaka mingine yote huwa tunakuwa na stock tani 30,000 mpaka kufikia Novemba lakini mwaka huu ajabu hatukuwa na stock kabisa,” alisema Ally.

“Yaani kila mnachokizalisha kinakwenda sokoni. Wastani wetu wa mauzo huwa ni tani 6,000 au 7,000 kwa mwezi lakini tulikuwa tunauza tani 12,000 kwa mwezi,” alisema Ally.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live