Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muswada wazipeleka Saccos, Vicoba na benki bubu kusajiliwa BoT

26595 Pic+bank TanzaniaWeb

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wajasiriamali wanaofanyabiahara ya kukopesha fedha kwa riba mitaani, sasa wajipange kulipa faini ya hadi Sh10 milioni au kwenda jela mpaka miaka mitano iwapo wataendelea bila kusajiliwa.

Hayo ni mapendekezo yaliyomo kwenye muswada wa sheria ya taasisi ndogo za fedha ambao uliwasilishwa na Serikali bungeni ili kujadiliwa kabla ya kuidhinishwa na kuanza kutumika.

Adhabu hiyo itatolewa kwa wajasiriamali hao ambao wamekuwa kwenye kundi la nne la taasisi ndogo za fedha, vikundi vya fedha vya kijamii maarufu vicoba na taasisi za fedha za kijamii.

Muswada huo unapendekeza adhabu tofauti kwa kila aina ya taasisi ndogo ambazo zimewekwa makundi manne.

Licha ya adhabu watakayopewa wajasiriamali binafsi, watoa huduma wengine waliomo kwenye kundi la nne, muswada unapendekeza kutozwa faini ya hadi Sh50 milioni au kifungo kisichopungua miezi mitatu na kuzidi miaka mitano.

Saccos zote zimo kwenye kundi la tatu wakati kundi la pili linajumuisha taasisi zisipokea amana za wateja na la kwanza ni taasisi ndogo zinazopokea amana za wateja, yaani benki ndogo.

Kwa watakaokiuka sheria, waliomo katika kundi la kwanza na la pili, muswada unapendekeza kutozwa faini isiyopungua Sh20 milioni lakini isiyozidi Sh100 milioni au kifungo kisichopungua miaka miwili na kisichozidi miaka mitano, au vyote viwili.

Kwa Saccos, zitatozwa faini ya hadi Sh50 milioni au kifungo kati ya miaka miwili hadi mitano au vyote viwili.

Adhabu hizo zinabainishwa katika kifungu namba 27 cha muswada huo na kufafanua kwamba hakuna anayeruhusiwa kufanya biashara ya huduma za fedha bila leseni husika.

Licha ya masharti hayo, muswada umeweka utaratibu wa kumlinda mteja dhidi ya riba kubwa inayotozwa kwa kuweka uwazi katika suala hilo, kuzingatia kanuni na viwango namna ya kukusanya na kulipa madeni yaliyopo.

Kama ilivyo kwa benki za biashara na taasisi za fedha, muswada huu unalenga kuipa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jukumu la kuzisimamia taasisi ndogo za fedha na wajasiriamali wanaotoa huduma hizo.



Chanzo: mwananchi.co.tz