Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mulamula, Mkumbo wasifu bidhaa, weledi TSN

61cf41b75b8cd51940b81e5fa9f81205 Mulamula, Mkumbo wasifu bidhaa, weledi TSN

Mon, 5 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, wamepongeza Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) kwa kazi nzuri inayoifanya kuhabarisha umma, bidhaa na weledi wa hali ya juu.

Walisema hayo walipotembelea banda la TSN kwa nyakati tofauti katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.

Balozi Mulamula alisema wizara hiyo ipo tayari kutumia bidhaa na huduma za TSN hasa ya kupata magazeti kidijitali (e-paper) inayowezesha mtu kusoma gazeti popote na kwa gharama ya nusu bei.

TSN ni wazalishaji wa gazeti la Daily News, Sunday News, HabariLEO, HabariLEO Jumapili, HabariLEO Afrika Mashariki, SpotiLEO na huduma za habari kidijiti kupitia tovuti, mitandao ya kijamii ukiwemo wa Daily News Digital.

Mulamula aliipongeza TSN na kuahidi kuongeza ushirikiano katika kuwatumikia wananchi na kutumia bidhaa za kampuni hiyo kutangaza zaidi kazi za wizara hiyo hasa huduma ya e-paper.

"Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya kuhabarisha wananchi na kuinua wizara yetu ya mambo ya nje," alisema.

Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa TSN, Prosper Mallya, alimueleza Waziri Mulamula kuwa, TSN imeendelea kuboresha huduma katika kuwafikia watu wengi zaidi ikiwemo kuweka nguvu katika kusoma gazeti mtandaoni.

Mallya alisema ofisi zote za za ubalozi wa Tanzania nje ya nchi na za nchi nyingine hapa nchini, zinaweza kutumia e-paper kusoma magazeti ya TSN kila siku na kupata taarifa sahihi na kwa wakati.

TSN pia inatoa huduma za ushauri wa kitaaluma, mafunzo, jukwaa la biashara, picha za biashara, maktaba na inafanya kazi kama wakala wa habari.

Awali, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, alisema TSN inafanya kazi nzuri na kwa weledi katika kuelimisha na kuhabarisha umma.

Profesa Mkumbo alisema hayo juzi Dar es Salaam alipotembelea banda la TSN DITF.

Alivitaka vyombo vya habari vya serikali viongeze bidii katika kazi kwa sababu serikali inaviunga mkono kwa asilimia 100.

Profesa Mkumbo alisema anafurahi kuona namna TSN inavyotimiza wajibu wake wa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kuleta maendeleo kwa Watanzania.

Mallya alimweleza kuwa, TSN inafanya kazi ya kuchapisha bidhaa nyingine kama vile majarida, vitabu, na kalenda.

Chanzo: www.habarileo.co.tz