Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mufuruki na wenzake wameshauri jinsi ya kufanikisha viwanda

20135 Pic+mufuruki TanzaniaWeb

Mon, 1 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mjadala wa ujenzi wa viwanda utakaoisaidia Tanzania kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ni hoja inayomvutia kila mpenda maendeleo.

Watu binafsi, kampuni na mashirika ya ndani hata kimataifa wametoa maoni yao juu ya nia hii njema ya Serikali kuboresha maisha ya wananchi wake.

Kwa nyakati tofauti wadau wa sekta ya viwanda wamekuwa wakijadili namna ya kufanikisha ushiriki wa Watanzania katika sekta ya viwanda huku Serikali ikiwa mstari wa mbele kuwashawishi kuingia kwenye uwekezaji.

Kampeni ya kushiriki imeendelea kupewa uzito nchini hata kuwaalika Watanzania waliopo nje kurejea ili kuzichangamkia fursa zilizopo katika viwanda na sekta zinazokabribiana nayo.

Haya yote yanafanywa ili kuona sekta hiyo ikitoa mchango mkubwa kufanikisha malengo ya dira ya maendeleo ya Taifa 2025.

Miongoni mwa wengi waliotoa maoni yao ni wakurugenzi wanne walioungana kuandika kitabu kiitwacho; Tanzania’s Industrialisation Journey 2016-2056 kinachotoa mapendekezo ya kuandaa sera zitakazohamasisha uchumi wa viwanda.

Kwa mtazamo wao, kwa miaka 50 ijayo, waandishi wa kitabu hicho; Ali Mufuruki, Rahim Mawji, Moremi Marwa na Gilman Kasiga wanasema ni muhimu Serikali ikafanya mapitio ya kina kwenye sheria, muundo wa taasisi kwa kuratibu na kufuatilia uongozi na mfumo uliopo.

Serikali inashauriwa kupima na kuja na mfumo mpya, wenye msukumo na nguvu utakaowezesha viwanda vinavyotarajiwa kujengwa pamoja na vilivyopo kufanikiwa.

Kwa kutumia uzoefu wao, mfanyabiashara mkubwa nchini, Mufuruki; ofisa mtendaji mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) Marwa; meneja wa maendeleo ya biashara wa kampuni ya General Electric, Kasiga na mwanafunzi wa shahada ya pili anayesona nchini China, Mawji wanasema wazalishaji wa ndani wanapaswa kulindwa dhidi ya ushindani hasa usio wa haki.

“Kama ambavyo mwanamasumbwi wa uzito wa chini hawekwi ulingo mmoja na mwenye uzito wa juu, mzalishaji mdogo hawezi kupambana na mzalishaji mkubwa tena kutoka nje. Wazalishaji wa ndani wakifikia hatua ya kushindana, msaada wa Taifa kuwalinda na kuwalea unaweza kupunguzwa ikionekana ni muhimu kufanya hivyo,” inasomeka sehemu ya kitabu hicho.

Kabla hawajaingia kwenye ushindani wa kimataifa, kitabu hicho kinapendekeza kwamba wazalishaji wa ndani wanahitaji kipindi cha kusaidiwa na kulindwa kwa na Serikali, wakati wakiimarisha uwezo wao wa kuzalisha.

Utaratibu maalumu

Kuna utaratibu maalum ambao Serikali inaweza kuutumia kuongeza ubora na ufanisi wa uzalishaji sanjari na kujenga uwezo wa wazalishaji wa ndani.

Kitabu hicho kinafafanua kuwa kuanzisha kwa utaratibu huo kutasaidia kuendeleza viwanda hususan vinavyochakata malighafi zinazopatikana Tanzania, vikilimikiwa na kuajiri Watanzania.

Waandishi wanawashauri wazalishaji kutumia zaidi malighafi zinazopatikana nchini badala ya kuagiza kutoka nje ili kupunguza gharama za uzalishaji na bei ya bidhaa husika sokoni hivyo kutoa unafuu kwa wananchi ambao ni wateja wake.

“Ikiwa kuna Mtanzania mwenye uwezo wa kufanya kazi kutoka chini hadi ngazi ya usimamizi na uendeshaji, mzalishaji amwaajiri Mtanzania na akikosa basi hatua zinazofaa zichukuliwe,” inanukuu sehemu ya kitabu hicho.

Kwa fani zenye uhaba wa wataalamu, kitabu hicho kinapendekeza wasio Watanzania waajiriwe kwa muda mfupi huku wazawa wakifundishwa wakijengewa uwezo wa kushika nafasi muhimu za kusimamia uchumi kwa kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wenye tija.

Kwa kuwa kila kitu kinafundishika, wazawa wafundishwe waandaliwe kwa mafunzo ya kina kujaza nafasi za wageni kwa kufuata mfumo utakaoratibiwa na wawekezaji kwa kushirikiana na Serikali.

Aidha, waandishi wameeleza ni muhimu kutunza kumbukumbu ili kila Mtanzania atakayelipiwa mafunzo na wazalishaji wenye viwanda, aajiriwe na kiwanda hicho.

“Ikiwa mzalishaji hawezi kukidhi mahitaji ya mipango ya ajira ya ndani na mfumo huu wa wageni kuwapisha wenyeji uliowekwa, basi Serikali haitatoa msaada juu ya mpango huu kwa mzalishaji husika,” kinasomeka kitabu hicho.

Ruzuku, msamaha wa kodi

Kuhamasisha uwekezaji hasa ujenzi wa viwanda, kitabu kinapendekeza kuwapo kwa ruzuku na msamaha wa kodi na kutoa mfano jinsi China inavyofanya hivyo kwa wazalishaji wake wanaouza bidhaa nje ya nchi.

Si China pekee, waandishi wanasema Marekani ni mfano mwingine makini wa jinsi Serikali inavyoweza kuwapa kipaumbele wazalishaji wake. Wanasema Marekani hutoa zaidi Dola 50 bilioni kwenye mfuko wa utafiti wenye wasomi wa vyuo vikuu kutafuta fursa mpya zilizopo.

Endapo suala hilo litaigwa na kutekelezwa kwenye sekta za kipaumbele mfano viwanda vy anguo na ngozi ambavyo malighafi zake hupatikana kwa wingi nchini, wanasema itakuwa rahisi kupiga hatua.

“Tanzania pia inaweza kufundisha mafundi wazuri wa nguo kuvutia wazalishaji wakubwa wa viwanda vya nguo. Ruzuku inaweza kujumuisha mikopo nafuu ya benki,” anapendekeza.

Makala yametafsiriwa kutoka kwenye kitabu cha Tanzania’s Industrialisation Journey 2016-2056

Chanzo: mwananchi.co.tz