Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtendaji GST azishawishi Slovakia, China kuwekeza kwenye uchimbaji wa madini

Dubai Pic Mtendaji GST azishawishi Slovakia, China kuwekeza kwenye uchimbaji wa madini

Tue, 9 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dk Musa Budeba ameishawishi Slovakia kuwekeza Tanzania kwenye uchimbaji au ununuzi wa madini ya viwandani.

Imeelezwa kuwa madini hayo hutumika kutengeneza vifaa vya teknolojia mbalimbali yakiwamo magari.

Dk Budeba ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 9, 2021, alipofanya kikao na mwakilishi kutoka Slovakia baada ya wataalam wa Tanzania kutembelea banda la nchi hiyo katika Maonyesho ya Kimataifa ya Expo 2020 Dubai yanayoendelea.

Amesema wataalamu hao walipata fursa ya kujionea teknolojia mbalimbali zinazozalishwa na nchi ya Slovakia likiwamo gari linalotumia hydrojeni.

Awali, akizungumza na Mkurugenzi wa Uchumi na Uwekezaji wa Kampuni ya Sario inayomilikiwa na Serikali ya Slovakia, Egon Zorad, Dk Budeba alisema Tanzania inayo madini ya aina hiyo ambayo ni malighafi katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani.

“Tumeona Slovakia imepiga hatua kwenye masuala ya teknolojia, mnatengeneza magari yanayotumia haidrojeni na tumeona mmetengeneza mifano ya ndege. Kwetu sisi kama sekta ni fursa ya kuwavutia mje kuwekeza kwetu kwa ajili ya kupata malighafi ya kutengeneza bidhaa zenu, kwa sababu vitu vyote tulivyoviona vinahitaji malighafi zinazotokana na madini kama nickel, copper, rare earth elements, graphite na mengine ambayo yote yapo kwetu,’’ amesema Dk Budeba.

Kwa mujibu wa Zorad, gari hilo ambalo limechukua takriban miaka mitatu kukamilika, limetengenezwa na vyuo vikuu vya nchini humo kwa kushirikiana na Serikali na kampuni binafsi.

Wakiwa kwenye banda hilo, Wataalamu hao kutoka Tanzania walielezwa jinsi nchi hiyo inavyojaribu kukuza teknolojia zake na kuhamia katika mifumo mingine ya kiteknolojia ambayo ni pamoja na matumizi ya magari yanayotumia umeme.

Hivyo, Dk Budeba amemuhakikishia mwakilishi huyo kuhusu upatikanaji wa rasilimali za kutosha yakiwemo mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara yaliyopo nchini kama ya usalama, na miundombinu ya kuwawezesha kufanya shughuli zao kikamilifu.

Amesema Tanzania inakusudia kuunganishwa na wawekezaji wengine wakubwa kutoka nchini Slovakia.

Akizungumzia kampuni ya kuunda magari, Dk Budeba amesema Tanzania itafarijika kama Slovakia itaanzisha kampuni ya uundaji magari nchini kutokana na uhakika wa upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika kuunda bidhaa hizo.

Amesema Tanzania tayari inayo kanzidata yenye taarifa za kutosha kuhusu uwapo wa madini hayo.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Sario, Zorad ameshukuru kukutana na kiongozi kutoka Wizara ya Madini na kufahamishwa kuhusu uwepo wa rasilimali wanazotumia katika kazi zao.

Hivyo aliomba kupatiwa taarifa za kutosha kuhusu masuala muhimu ya uwekezaji na biashara ya madini Tanzania kwa lengo la kutaka kuiunganisha Tanzania na kampuni nyingine zilizoko Slovakia.

“Nataka sana Tanzania kuwa moja ya nchi tutakayoshirikiana nayo kwenye biashara na vyuo vyetu. Tumeelezwa nchi yenu iko kwenye nafasi nzuri kibiashara hasa kwenye masuala ya madini. Slovakia tunaandaa mkutano wa wawekezaji, tunatarajia kualika angalau nchi moja kutoka Afrika na haina shaka itakuwa Tanzania,’’ amesema Zorad.

Mbali na masuala yanayohusu madini, pia, mwakilishi huyo wa Kampuni ya Sario, amesema Slovakia inapenda kushirikiano na vyuo vikuu vya Tanzania hususan kwenye masuala ya utafiti.

Wakati huohuo, maafisa wengine wa Wizara ya Madini walifanya mkutano kwa njia ya mtandao na mwekezaji kutoka China aliyetaka kuwekeza nchini kwa kushirikiana Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Hivyo, Dk Budeba alimuunganisha mwekezaji huyo na Kaimu Mkurugenzi wa Stamico kwa hatua zaidi.

Naye Mkurugenzi wa Banda la Tanzania kwenye Maonyesha haya ya Expo 2020 Dubai, Getrude Ng’weshemi ameendelea kusisitiza ushiriki wa uhakika kama huu kwa sekta nyingine ambazo zinatarajiwa kushiriki maonyesho.

Amesema lengo ni kutaka kuona Tanzania inatumia vilivyo fursa zilizopo Dubai na kwingine duniani kupitia maonyesho hayo.

Chanzo: mwananchidigital