Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtanzania kidedea shindano ubunifu wa teknolojia

Mtanzaniapic Data Mtanzania kidedea shindano ubunifu wa teknolojia

Fri, 10 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mtanzania Godfrey Kilimwomeshi ameibuka kidedea kwenye shindano la kazi za ubunifu wa teknolojia lililohusisha nchi tano za kusini mwa Afrika.

Shindano hilo linaloratibiwa na programu ya kukuza ubunifu kusini mwa Afrika (SAIS) lilifanyika nchini Finland ambayo ndiyo nchi mfadhili.

Kilimwomeshi ameshinda baada ya kuwagaragaraza washiriki wengine kutoka nchi za Afrika Kusini, Botswana, Namibia na Zambia.

Kupitia ubunifu wake wa mfumo wa simu (mobile app) unaowawezesha wenye mahitaji ya ufundi kupata huduma hiyo kupitia simu ya mkononi.

Akizungumza leo Ijumaa Desemba 10, 2021 Kilimwomeshi amesema kupitia shindano hilo ambalo limewawezesha kunadi kazi zao mbele ya wadau wa teknolojia na tayari wawekezaji wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye ubunifu wake.

“Imekuwa ni fursa ya aina yake, kwani kushindanishwa na nchi ambazo zimeendelea kiteknolojia halafu bado majaji wakaona kazi yangu ndio bora, sio kitu kidogo.

Advertisement “Pia kuna wawekezaji watatu tayari wameshaonyesha nia ya kuwekeza kwenye ubunifu wangu jambo ambalo linanipa matumaini makubwa ya kufanya vizuri zaidi,” amesema Kilimwomeshi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Sayansi Tanzania (Costech), Dk Amos Nungu amewataka vijana wenye kazi za bunifu kutohofia kushiriki mashindano ya kimataifa kwani ni fursa ya kujitangaza.

“Kama nchi tuna kila sababu ya kujivunia ushindi huu kwa kuwa umeiweka Tanzania katika nafasi ya kufahamika kimataifa.

“Niwashauri wabunifu kuchangamkia fursa zinazotolewa na tume, kuna fursa nyingi za kuendeleza ubunifu msiziache zipotee zichangamkieni,” amesema Dk Nungu.

Kuhusu SAIS amesema mradi huo umekuwa ukitekelezwa nchini kwa mwaka wa nne na unatarajiwa kuhitimishwa mwakani.

Kando na Kilimwomeshi mshiriki mwingine wa Tanzania aliyeshiriki kwenye shindano hilo ni mwanafunzi wa kidato cha tatu Moses Mbaga.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz