Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtanzania anavyoongeza mapato Sudan Kusini

906108d1587ffbcab151e00e594fa3c2 Mtanzania anavyoongeza mapato Sudan Kusini

Tue, 26 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MTANZANIA aliyeajiriwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Sudan Kusini, Dk Patrick Mugoya amesema kwa kipindi kifupi alichoshika nafasi hiyo amefanikiwa kuongeza mapato ya nchi hiyo kwa asilimia 10.

Amesema kwa wastani makusanyo ya robo ya pili ya mwaka 2020/2021 yaani kuanzia Oktoba mpaka Desemba, mwaka jana yalikuwa zaidi ya asilimia 220 ya wastani wa makusanyo ya mwezi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha yaani Julai – Septemba, mwaka jana.

Akizungumza na HabariLEO Afrika Mashariki akiwa Sudan Kusini, Dk Mugoya alisema ni vigumu kupima mafanikio kwa muda mfupi, lakini kwa kushirikiana na wafanyakazi wenzake wa mamlaka hiyo wameanza kuchukua hatua za muda mfupi na kati za kusimamia makusanyo ya fedha za serikali na matunda yameanza kuonekana.

“Mafanikio haya makubwa ambayo kwa sasa ni gumzo kubwa ndani ya serikali, ni matokeo ya moja kwa moja ya hatua ambazo tumezichukua mara tu nilipoingia ofisini Oktoba, 2020 za kudhibiti misamaha holela ya kodi, usimamizi wa karibu wa uwasilishaji ritani za kodi za kila mwezi kwa kuanza kidogo kidogo kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT),” alisema.

Alisema usimamizi wa maadili kwa wafanyakazi na kufanya mabadiliko kidogo ya uongozi wa kati na kuanza kuhamasisha walipa kodi na umma kwa ujumla juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari ni miongoni mwa njia zilizoleta mafanikio.

“Kwa sasa mimi na wasaidizi wangu tunaendelea na maandalizi ya kimkakati ya maboresho ya kisera na kiutawala ambayo nina imani ndani ya muda wa kati yataleta matokeo makubwa chanya na ya kimapinduzi katika tasnia ya ukusanyaji wa mapato ya serikali nchini Sudan Kusini,” alisema.

Akizungumzia jinsi alivyopata nafasi hiyo, Dk Mugoya alisema ilitangazwa ilitangazwa kimataifa na yeye alipojitathmini kulingana na vigezo vyao aliwasilisha maombi.

“Vigezo vyao muhimu vilikuwa pamoja na elimu ya walau shahada ya uzamili kwenye masuala ya kodi, uzoefu kwenye utawala wa kodi katika ngazi za juu za uongozi, uzoefu wa kazi katika mazingira ya nchi changa hususan zilizowahi kukumbwa na migogoro, uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya utengamano wa Afrika Mashariki na uadilifu,” alisema.

Alisema takribani watu 12 kutoka mataifa mbalimbali akiwemo walikuwa na vigezo hivyo na ndipo wakapelekwa kwenye mchakato mrefu wa usaili uliosimamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na yeye kuibuka mshindi na kukubaliwa na Serikali ya Sudani Kusini na kuteuliwa kushika wadhifa huo kuanzia Oktoba, mwaka jana.

Alisema mifumo ya kodi ya Sudan Kusini na Tanzania ina tofauti kwa viwango vya kodi, ambapo Sudan Kusini viko chini ikilinganishwa na Tanzania.

“Mathalani kiwango cha juu cha kodi ya mauzo kule Sudan Kusini ni asilimia 10, wakati kwa kodi ambayo ni mbadala wa hii yaani Kodi ya Ongezeko la Thamani huko nyumbani ni asilimia 18,” alisema.

“Wakati kiwango cha juu cha kodi ya mapato Tanzania ni asilimia 30, nchini Sudan Kusini ni asilimia 20 na hakuna Kodi ya Ongezeko la Thamani ambayo ni muhimu katika kupanua wigo wa kodi hususan kwenye nchi za ulimwengu wa tatu kama hii,” alisema.

Dk Mugoya alisema matumizi ya ICT kwenye ukusanyaji wa mapato ya serikali Sudan Kusini yapo chini ikilinganishwa na Tanzania.

Alitaja majukumu yake kuwa ni pamoja na kuishauri serikali kuhusu sera muafaka zinazohusiana na eneo la kodi, usimamizi wa siku kwa siku wa shughuli za mamlaka hiyo yakiwamo masuala ya fedha na rasilimali wat una uandaaji wa mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Alisema kwa muda mfupi aliokaa nchini humo, ameona Watanzania wachache wakiwa na shughuli mbalimbali tofauti na wananchi wa mataifa mengine jirani wanaofanya shughuli zao za kujiajiri au kuajiriwa.

Chanzo: habarileo.co.tz