Dar es Salaam. Mtafiti wa Masuala ya Kilimo wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Dk Anna Temu amesema kuna haja ya kuangalia kwa undani suala la masoko ili kilimo kiweze kufanya vizuri nchini.
Dk Temu ametoa kauli hiyo, leo Alhamisi Mei 23,2019 wakati akizungumzia suala la msaada na huduma kuhusu sekta ya kilimo katika mjadala wa Jukwaa la Fikra uliokuwa na mada ya ‘Kilimo, Maisha yetu’ ulioandaliwa kampuni ya Mwananchi Communication ltd (MCL) ikishirikiana na ITV na radio One.
Jukwaa hilo la nne linahudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na wadau wa mbalimbali wa maendeleo na kilimo , likiwamo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (FAO).
Dk Temu ametaja masoko hayo kuwa ni la ardhi, rasilimaliwatu, teknolojia na huduma za ugani akisema yakitiliwa mkazo kilimo kitafanikiwa.
“ Kuna haja ya kuangalia soko la rasilimaliwatu, lazima tujue vijana tulio nao uwezo wao kwenda kwenye kilimo. Soko la wajasiriamali watu tulilonao haliwezi kuwafikia wakulima kwa ufanisi,” amesema Dk Temu.